DALILI ZA MWANAMKE ANAYEKUPENDA
(ukiwa
naye katika mahusiano)
1. Utaona mabadiliko katika muonekano
wake. Ukitaka kumfahamu msichana ambaye yupp katika mapenzi kama alikuwa
hajipendi pendi kwa maana kuwa rafu hata akiwa katika mazingira ya nyumbani
basi katika kipindi hiki atakuwa msafi kuanzia nguo, nywele ataweka kila staili
itakayompendeza atafanya kila kitu ili kukuvutia.
2. Anajali kama mwanamke anakupenda
atakujali hatopenda kuwa mbali na wewe kama atagundua upo katika tatizo.
Atakufanya ufahamu yupo kwa ajili yako pale utakapomhitaji.
3. Anajitoa kwa ajili yako. Atachukua
muda wake hata wa maana kuwa na wewe atafanya vitu ambavyo unavipenda na
kuviacha vya kwake pale inapobidi
4. Huwa muwazi kwa kila anachokifanya
nini anapanga kufanya na nani anakutana naye kwa wakati gani.
5. Wewe ni mvulana pekee anayetazamia
uje kuwa mume wake anazungumzia mambo mengi kuhusu maisha ya baadaye kama vile
ndoa watoto wangapi mzae pamoja na familia tenu iwe vipi
6. Anapenda kuwa na wewe muda mwingi.
Msichana mwenye mapenzi hufanya haraka kumaliza ubusy wake ili asipoteze muda
mwingi akashindwa kukuona tena kwa siku hiyo. Anaweza kuacha hata shughuli zake
ili aje kukaa na wewe hata kama mkutano wenu hauna maana na faida kwake.
7. Anakushika kwa hisia
msichana mwenye mapenzi huwa na hisia ndio maana hupenda kushijka kila sehemu yako ya mwili kwa hisia za kweli akijitaji na wewe uhisi anachohisi kupitia mguso wake.
msichana mwenye mapenzi huwa na hisia ndio maana hupenda kushijka kila sehemu yako ya mwili kwa hisia za kweli akijitaji na wewe uhisi anachohisi kupitia mguso wake.
8. Atakutambulisha kwa ndugu jamaa na
rafiki zake hupenda kila mtu wake wa karibu akufahamu hivyo hupenda
kukutambulisha kwa kila mtu haoni aibu kufanya hivyo kwa kuwa anatarajia
utakuwa wake wa kudumu
(wale ambao
tunachelewa kujibu msg zenu naomba mtuvumilie tutawajibu mapema na mada zenu
tutaziweka pia, ikikupendeza hii unaweza kushare pia) baadaye tutawaletea vitu
ambavyo wasichana hawapendi kuvisikia wawapo kitandani na wapenzi wao
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
NJIA ZA KUFANYA UPENDWE NA WATU WA MAANA
KUPENDWA ni sawa, lakini kupendwa na mtu wa maana ni
jambo zuri zaidi katika maisha ya Mwanadamu yeyote yule.Kupendwa na mtu ambaye
lengo lake ni kukupotezea muda, si jambo linalofaa hata kidogo.
Kuna na mpenzi ambaye hata kwao hataki kukupeleka,
kuendelea kuwa naye ni sawa na wewe kuwa mjinga.
Mpenzi ambaye unapaswa kuwa naye ni yule ambaye si
tu kwamba anao uwezo wa kukupeleka kwao, lakini pia awe mwenye uelekeo wa
kufunga ndoa na wewe.
Ukiwa na mpenzi ambaye hana maana thabiti ya kuwa
nawe, hakika nakwambia uhusiano huo haufai. Ndugu zangu maisha ni mafupi kwa
maana hiyo ni lazima uwe makini katika maamuzi yako, acha kuwa na mtu ambaye
anakupotezea muda tu.
Kama uko kwenye uhusiano unapaswa kutafakari kwa
makini kama ni lazima kuendelea na uhusiano huo. Jinsi ya kuona kama unapaswa
kuendeleza uhusiano huo au la, ni kuangalia kama ni uhusiano ambao unalengo la
kudumu au la muda mfupi au pengine hata hauna malengo yoyote ya maana.
KUPENDA NA HISIA
Katika maisha wakati mwingine inaweza kutokea
umempenda fulani, wapo ambao wana uwezo wa kueleza hisia zao, lakini pia wapo
ambao hawana uwezo wa kufanya hivyo kwa uwazi.
Kubaki na hisia au kuzitoa haliwezi kuwa ni suala la
moja kwa moja kama ni suala jema au la, cha msingi sana ni kutafakari kwa
makini kile ambacho unakiona kwa mbele yako.
Wakati mwingine si sahihi kuficha hisia hasa kama
umefanya utafiti wako na kubaini kwamba mtu huyo ni mzuri kwako.
1.KUONYESHA UKOMAVU
Watu hupenda wenza ambao wanaonyesha ukomavu katika
kushughulikia changamoto mbalimbali za maisha, kiasi kwamba unaweza kujiona
kwamba kweli ninaye mtu ambaye hata kukiwa na jambo la hatari hataweza kuyumba.
Mwenza ambaye anajiwekea mikakati katika kuinua kipato chake.
2. UWEZO KATIKA MAHABA
Kuna watu wanaamini kwamba wanawake walio wengi
wanampenda fulani kwa sababu ya fedha au mali zake. Imani hii haina ukweli
wowote, ukweli ni kwamba watu wanachohitaji katika maisha ni mtu wa kumpenda
kwa dhati na kumpa raha thabiti.
Ndio maana ndugu yangu nafikiri utakuwa shahidi,
unaweza kuwa na mtoto unampa kila kitu, lakini bado anaruka ukuta na kwenda kwa
mwenza wake, anafuata fedha? Anafuata nini? Jibu unalo.
Kwa maana hiyo inaonyesha ni kwa namna gani maisha
ya uhusiano hayaendeshwi sana na fedha, bali furaha ya dhati.
Mwanamke kwa mfano anahitaji kupendwa, kutia raha
ambayo anaisikia kwa wanawake wenzake. Lakini zaidi ya yote kama uko katika
mahaba na mwanamke, ni kosa kubwa mwanaume kufikia mwisho, kabla ya mwanamke.
Kitaalamu ili raha ya mahaba iwepo ni lazima kwanza aanze mwanamke, kisha
ufuatie mwanaume.
3. MWAMINIFU
Mwenza ambaye kwa mfano simu yake muda wote hawi na
mashaka nayo, wala haoni ulazima wa kuweka namba za siri kwenye simu yake, huyo
anafaa.
Ikiwa una mwenza ambaye simu yake imejaa namba za
siri (password)....pole! Mtu anaweza kubisha kwa sababu za kutetea ujinga wake,
lakini kwa asilimia kubwa ni ishara mbaya.
Endelea kuomba Mungu akusaidie, lakini kwa kweli
hapo iko shida. Mwanamke au mwanaume ambaye ni mwaminifu, hana masharti kwenye
simu yake, kiasi kwamba hata anapolala, simu haizimi, bali anaweka kwenye
kitanda na kupunguza sauti.
Kutokuzima simu kuna faida hasa usiku. Kuna dharura
au uvamizi wa majambazi, majirani wanaweza kuwapigia simu na kuwaeleza
kinachoendelea huko nje. Lakini kwa sababu ya kutokuwa na uaminifu, wengi
wanazima simu au kuzificha wakati wa kulala.
4. KUTUMIA WAKATI PAMOJA
Kama wapenzi, jambo ambalo linafurahisha ni kuona
wanakuwa pamoja wakati fulani kama vile kwenye matembezi ya kawaida.
Ndio kusema kwamba kama kweli unataka kuimarisha
uhusiano wako, ni lazima kuangalia namna gani unakuwa karibu na mwenza wako,
kinyume na hicho unaruhusu mabaya kujitokeza.
5. KICHEKO
Unapokuwa na mwenza wako, penda kufurahi nae, cheka
nae.
6.MATENDO YA KUFURAHIANA
Ni kweli inawezekana uko bize sana katika kazi, ni
jambo la msingi kwa wapenzi kutenga muda wa kuonyesheana upendo.
9. KUELEMISHANA
Inawezekana kuna jambo ambalo wewe unalifahamu,
mwenza wako halifahamu, jitahidi kumwelimisha pole pole ili aweze kulielewa.
Hakuna mtu aliyekamilika kwa asilimia 100, cha msingi ni kuwa makini na namna
ambavyo unamwelemisha mwenza wako.
Zaidi ya yote pendelea kusema nenoNAKUPENDA.
. Hata hivyo kusema nakupenda pekee haina maana kama
hutafanya mambo kwa vitendo. Kumwambia mtu nakupenda, wakati unamtesa ni sawa
na upumbavu
xxxxxxxxxxxxxxxxxUSIISHI KWA DHANA
UKIISHI kwa dhana
kwenye mapenzi, tena dhana mbaya utaharibikiwa mapema. Kama ndoa haikukushinda
basi itakumbwa na migogoro isiyokwisha.
Hisia mbaya kwa
mwenzako, kuamini kila baya unaloambiwa kumuhusu mwandani wako, kuchunguza kila
afanyalo mwenzako, ni dalili za kuishi kwa dhana na hilo si jambo jema sana
katika maisha ya kimapenzi.
Mkeo akikuaga nakwenda
saluni kusuka nywele humuani, unamfuata nyuma kimya kimya. Akichelewa sokoni
unazusha zogo kwa kudhani amepitia kwa wale wenyewe wanaita ‘kidumu.’ Hayo ni
maisha ya kujitesa na yasiyofaa katika ndoa.
Wapo baadhi ya wanaume
tangu asubuhi wanapong’oa mguu nyumbani mpaka usiku wanapourudisha, simu zao
haziishi kuita. Anayepiga kila mara si mwingine bali ni mke.
Mwanamke huyu hapigi
kwa kumjulia hali mume, au kwa kujawa na penzi la dhati, bali anapiga kwa madai
ya kudhitibi mume. Anapiga kila wakati kujua mumewe yuko wapi, yuko na nani na
unafanya nini! Anapiga akiamini hiyo ndiyo njia muhimu ya kumdhibiti mumewe
asitoke na wanawake wengine.
Wapo wenzangu wake zao
wakichelewa mahali fulani, wakirudi nyumbani wanawavua chupi kuwachunguza kwa
dhana labda wamepitia kwa hawala. Huku ni kujitesa na wala huwezi kuyaita
mapenzi.
Kama unaamini mumeo au
mkeo si mwaminifu kwa kiasi hicho, basi ni bora ukaamua kuachana naye kuliko
kuishi kwa mateso namna hiyo. Dhana za namna hiyo hazijengi penzi lililo bora.
Tuelewane hapa.
Nazungumzia dhana – kumdhania mwenza wako jambo baya bila kuthibitisha na wala
sizungumzii wivu. Kuna tofauti kubwa kati ya dhana na wivu. Wivu katika mapenzi
unakubalika ingawa sio wivu uliopitiliza.
Ukiwa unahakika mkeo au
mumeo anatoka na mtu mwingine na ukaamua kufuatilia nyendo zao kwa lengo la
huwadhibiti hiyo sio dhana bali huo ni wivu na unakubalika. Lakini ukamkataza
mkeo asifanye kazi kwa kuamini akiwa kazini atatongozwa, huo sio wivu bali ni
dhana na haikubaliki.
Wapo wanaume
wanaowazuia wake zao wasifanye kazi, wengine wanawazuia wasijiendeleze kielimu
kwa dhana ya ‘kuibiwa.’ Wanahisi wakifanya kazi wakiwa na fedha au wakiwa na
elimu kuwazidi wao watawadharau na pengine kunyang’anywa.
Sikatai, yapo matukio
yanayofanana na hayo, lakini si busara kosa la mtu fulani ukamhukumu mtu
mwingine. Binaadamu hachungwi kama mbuzi bali anatakiwa ajichunge mwenyewe.
Ukiona mtu anafanya
vitendo vinavyomlazimisha achungwe kama mbuzi ujue mtu huyo hafai kwenye ndoa
au anafanya makusudi ili apate sababu za kuvunja ndoa yake.
Sisemi wanandoa wapeane
uhuru uliopitiliza, hapana. Natambua kuwa
uhuru wowote una mipaka yake, lakini kumnyong’onyesha mwenza wako kwa
dhana tu si jambo jema.
Rafiki yangu mmoja wa
Kigamboni Dar es Salaam ameingia kwenye dhana mbaya kwa mkewe. Ananiambia siku
akicha elfu tano nyumbani kwake anakuta pamepikwa wali na ‘mboga saba,’ lakini
siku akiacha elfu kumi anakuta pamepikwa ugali na maharage – anatia shaka.
Kijana huyu amekuwa
msomaji na mchangiaji wa safu hii kwa siku nyingi. Nafahamu kwamba ndoa yake
haina muda mrefu, inawezekana hajaelewa ratiba za mapishi ya mkewe maana
wanawake wengi huwa na ratiba ya vyakula watakavyopika kwa wiki mzima.
Inawezekana siku ambayo
rafiki yangu anaacha elfu tano ndiyo siku ya ratiba ya kupikwa ‘mchele’ na mama
hapangui ratiba yake sababu ‘mwekundu’ aliyoachiwa jana imebaki kwa kuwa jana
hakuwa na matumizi makubwa. Si alipika ugali na ndondo!
Nakushauri swahiba ukae
na mkeo umuulize kwa upole, naamini utaelimishwa na utaelewa na hatimaye, dhana
yako ya kusaidiwa matumizi itakuondoka.
Tusiishi kwa dhana.
Aloyce A, Nanyunga wa Bagamoyo Pwani, anatamani kujua anachofikiri mpenzi wake juu ya uhusiano wao wa kimapenzi.
Anataka kujua kama mpenzi aliyenaye ana mapenzi ya dhati kwake au laa. Anatamani kujua iwapo akifunga naye ndoa atamuheshimu au heshima ndio itaishia kwenye uchumba.
Aloyce anasema hapendi kuona ndoa yake inaingia kwenye migogoro ya mke na mume. Anataka ndoa yenye upendo na iliyotawaliwa na amani.
Anachotamani Aloyce kwenye ndoa yake ndicho wanachotamani wachumba wengi, wavulana na wasichana. Ukiwa kwenye uchumba unapatwa na mawazo mengi yaliyojaa wasiwasi kuhusu mchumba wako.
Wasiwasi wa kudanganywa na au kupachikwa mimba kisha kuachwa njiani ni kawaida sana kwa wasichana wenye kujithamini. Wanayafikiria hayo kwa kuwa ni kawaida sana kutokea kwenye jamii.
Kuna jambo moja ni muhimu Aloyce na wasomaji wengine, hasa wale wanaotarajia kuingia kwenye ndoa wakalifahamu. Kwamba, kutofautiana baina ya mke na mume ni jambo la kawaida na sio rahisi kuepuka.
Kugombana au kutofautiana baina ya wanandoa kwa jambo fulani si mgogoro; bali mgogoro ni pale jambo hilo linapojirudia mara kwa mara.
Kwa mfano; kuna jambo ambalo mume analifanya, lakini mkewe halipendi na mara kwa mara huwa wanagombana kutokana na mwanaume kurudiarudia kosa hilo. Huo tunaita mgogoro unaoweza kuhatarisha ndoa.
Kadhalika jambo analolifanya mke lakini mumewe halipendi na hata kila anapomuonya bado mke anarudia kosa hilo, huo nao ni mgogoro unaoweza kuvunja ndoa. Wahenga wanasema “kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa.”
Pia wasomaji wafahamu kuwa sio rahisi kujua kinachofikiriwa na mtu mwingine, hasa kama mtu huyo hujamzoea. Lakini kama utaishi naye kwa muda mrefu na kumzoea, angalau unaweza kuhisi anachofikiri, hasa kama utazingatia matendo yake.
Mtu anaweza kuficha tabia yake kwa muda mfupi, hivyo kama hutakuwa makini katika muda mfupi uliyokutana naye unaweza usipate undani wa tabia yake, lakini kama utaishi naye kwa muda mrefu unaweza ukagundua tabia yake kwa kuzingatia anavyoongea na anavyotenda.
Unaweza ukajua anachofikiri mtu wako wa karibu kwa kusikiliza kwa makini mazungumzo yake na kuangalia matendo anayotenda. Wakati mwingine anaweza akawa anaongea kwa mzaha na hivyo usipate tafsiri sahihi ya anachofikiri.
Hivyo basi baada ya kusikiliza anachokiongea, endelea kufuatilia matendo yake, hapo unaweza kukipata anachofiri juu yako, maana wakati mwingine wachumba wengi wanachokiongea sicho wanachokitenda.
Kama na matendo yake hayatakuridhisha kujua tabia halisi ya unayetaka kumchunguza, basi fuatilia matokeo ya maisha yake ya huko nyuma.
Ingawa si vizuri kumhukumu mtu kwa historia yake, lakini historia ya mtu ni muhimu sana katika kutambua matendo na hatimaye tabia za mtu.
Kawaida ya mwanadamu fikira zake ndizo huzaa maongezi, maongezi nayo huzaa vitendo na vitendo ndio hutoa matokeo ya yote, kwa maana ya fikira, maongezi na matendo.
Hata katika maisha ya kawaida, matokeo mazuri au mabaya ya maisha ya mtu hutegemea matendo yake aliyotenda. Matendo nayo hutegemea maongezi ya mtu na maongezi yanatokana na mtu anavyofikiri.
Mfumo uko hivi: Unavyofikiri – Unavyoongea – Unavyotenda – Matokeo.
Ndugu zangu, siku zote mapenzi na heshima ya mtu ni kama pembe – haifichiki. Anayekupenda lazima ataonyesha mapenzi yake kwako na anayekuheshimu lazima utamuona.
Mapenzi na heshima visipo kuwepo huna haja ya kutafuta mtaalamu wa kukutambulia, mwenyewe utaona bila kuambiwa.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Ndoa hailindwi kwa utaalamu wa kitandani
NDOA hailindwi kwa utaalamu wa kitandani.
wasichana waliovunja ungo wakati huo walikuwa wanaelezwa kwa undani juu ya kilichowatokea na kufundishwa jinsi ya kujiweka wasafi wa miili yao, nguo na mazingira wanayoishi.
Makungwi waliwafundisha vijana wao jinsi ya kuheshimu wakubwa na zaidi wakafundwa namna ya kuepukana na vijana wezao wa kiume ambao kwa wakati huo waliambiwa ni hatari kwao.
Sihishi kwa wasichana waliovunja ungo pekee, bali nikafika mbali kwa kusema unyago ulitumika pia kuwafunda wasichana waliotarajia kuolewa jinsi ya kuishi na mume pamoja na familia za
siku hizi mafunzo ya unyago yaliyokuwa yanatolewa kwa zaidi ya mwezi, tena kwa siri baina ya mwalimu na mwanafunzi wake yameondoka na kuingia kitu kipya kinachoitwa ‘kitchen party’ kinachofundishwa ukumbini huku halaiki ya watu wakishuhudia.
Katika sehemu hii ya pili, kwa uchache tunaendelea kuangalia faida walizopata wasichana waliopitia mafunzo ya unyago na hasara wanazopata wasichana wa sasa wasiopiti unyago.
Waliopitia unyago haikuwa rahisi kuona wakiacha miili yao wazi ili kila mwenye macho barabarani aone. Walijiheshimu; wakavaa nguo za heshima zenye kustiri miili yao.
Ilikuwa nadra sana kuona titi la msichana, tofauti na sasa ambapo huwezi kupanda daladala bila kuona titi lililoachwa wazi makusudi.
Waliopitia unyago walifundwa uvumilivu kwenye ndoa, tena kwa kutolewa mifano ya wazazi wao ambao waliishi miaka mingi bila kutengana.
Waliopitia unyago wanajua mwiko wa wanandoa kutotoa siri za ndoa zao. Kutoa siri za ndoa zao waliambiwa ni sawa na kuwatukanisha wazazi. Aibu!
Waliopitia unyago walifundishwa upole, unyenyekevu na heshima katika ndoa zao. Waliambiwa wanandoa hawagombani barabarani, wakikoseana wanasubiri wakiwa chumbani ndio wanakosoana.
Wasichana walifundishwa kutokuwa na ubia katika ndoa zao. Waliambiwa hakuna mbadala wa waume zao wala mbadala wake zao.
Waliambiwa marafiki wengi wanatakiwa waishie nje ya nyumba na wachache waishie sebuleni lakini hakuna rafiki mwenye mamlaka ya kuishia chumbani. Siku hizi kila rafiki ana uhuru wa kuingia anakotaka na kwa kuwa wengi wana chumba kimoja si ajabu wakapanda vitandani!
Waliopitia unyago walifundishwa na kuambiwa kuolewa pekee hakutoshi, bali kuna kazi kubwa ya kutunza ndoa.
Mafunzo hayo siku hizi hakuna kwa kuwa vicheni pati vya sasa kazi yake kubwa ni kukusanya vyombo tu basi. Haiwezekani msichana anayetarajiwa kuingia kwenye majukumu mapya na mazito akafundwa kwa saa moja tu, tena kwenye umati wa watu.
Wengine wanasema utamfunda nini mtoto wa kike wakati kila kitu anakijua, kabla ya kuingia kwenye ndoa. Si kweli kama kila kitu anakijua.
Hata kama ni mtaalamu wa kulala na wanaume lakini hakumsaidii kutunza na kulinda ndoa yake. Ndoa hailindwi kwa utaalamu wa kitandani isipokuwa kwa mafunzo maalum, ndiyo maana nashauri turudishe unyago ili kujifunza namna ya kulinda ndoa.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Jiulize maswali kabla hujaacha
UNAWEZA ukashikwa na hasira kali kutokana na mwenza wako kukutendea jambo fulani baya. Kwa hasira zako ukatamani kuachana naye kwa kufikiri unaweza kupunguza maumivu ya moyo.
Lakini wengi walio acha kwa hasira za ghafla hawakufanikiwa kutuliza maumivu ya moyo waliyotaraji kuyapunguza, bali wameongeza maumivu.
Iwe umemfumania mpenzi wako au amekufanyia kosa jingine lolote lililokupa maudhi yaliyokufanya uamini hakuna adhabu nyingine anayostahili zaidi ya kuachana naye, kwanza jipe majibu ya maswali haya machache kati ya mengi kabla ya kutoa maamuzi.
1. Jiridhishe na makosa
Kabla ya kuamua kudai talaka au kutoa talaka unapaswa ujiridhishe na makosa aliyoyafanya unayetaka kuachana naye. Lazima uhakikishe usahihi wa kosa alilofanya.
Na kama kosa hilo linajirudia mara kwa mara au imekuwa kawaida yake kufanya makosa yanayofanana na hilo , unaweza kuchukua hatua kali. Lakini kama ndio kosa la kwanza kulifanya basi msamaha unaweza kutumika na maisha yakaendelea. Wahenga wanasema “kosa la kwanza haliachi mke.” Nami naongeza, pia kosa la kwanza halidaiwi talaka.
Kuna umuhimu wa kujiridhisha kuwa, kosa alilofanya mwenza wako wewe huwezi kulifanya. Kama unashaka au una hakika kosa kama hilo nawe unaweza kulifanya au umeshalifanya, fikiria mara mbili kudai au kutoa talaka.
Kwa mfano; unaweza ukamfumania mkeo au mumeo na ukaona maamuzi sahihi ni kuachana naye. Hebu jiulize kabla ya kutoa adhabu hiyo; je, wewe hujawahi kutoka nje ya ndoa?
<!--[if !supportLists]-->2. <!--[endif]-->Umejiridhisha utampata wa kuziba pengo lake
Umejiuliza kwamba usipoyapata itakuwaje. Umejiuliza kwamba huyo atakayechukua nafasi anaweza kuwa kituko kuliko uliyenaye sasa. Umepata jibu la akiwa hakufikia hata nusu ya ubora wa unayetaka kuachana naye utafanya nini na hasa ikiwa kumrudia wa zamani haiwezekani.
<!--[if !supportLists]-->3. <!--[endif]-->Ni kweli hutamuhitaji tena
Usiache kwa shingo upande. Kabla hujaamua kuandika au kudai talaka lazima ujiulize na kupata jibu la swali hili. Je, ni kweli mkeo au mumeo hutamhitaji tena katika maisha yako?
Ukipata jibu la ndio hutamhitaji tena. Hapo unaweza kuendelea katika harakati zako za kudai au kutoa talaka.
Lakini iwapo jibu lako litakuwa hapana. Nitamhitaji au jibu likiwa SIJUI, tafadhali usithubutu kudai au kutoa talaka. Utakuja juta. Na Wahenga walisha tangulia kusema kwamba “majuto ni mjukuu.”
<!--[if !supportLists]-->4. <!--[endif]-->Uko radhi huduma anazokupa akampe mwingine
Hapa ndipo panapo wafanya watu watoane roho kwenye mapenzi. Baadhi ya wanandoa wakijua wenza wao wametoka nje ya ndoa, na wakawajua walio watendea uovu huo, wanadhani hukumu wanayostahili ni kuwatoa roho.
Maumivu makali wanayoyapata wanandoa wanapogundua kuwa wenza wao wametoka nje ya ndoa yanatokana na haswa tendo lenyewe – tendo la ndoa.
Watu wanavuta hisia wakati wao wakiwa na wapenzi wao kwenye maeneo yao ya kujidai (faragha). Mwanandoa akihisi mwenzake ametoka nje ya ndoa anafikiria vile ambavyo yeye anafanyiwa wakiwa faragha.
Sasa basi, wewe unayetaka kuacha au kudai talaka, umeridhika utamu unaopewa wewe, staili unazopewa na masham sham unayopewa apewe mwenzako. Kutimbwilika anakotimbwilika kwako uko radhi akamtimbwilikie mwengine? Jipe majibu ya maswali haya kabla kuamua kudai au kuandika talaka.
Haya ni baadhi tu ya maswali unayopaswa kujiuliza na kuyapatia mjibu kabla ya kuchukua hatua ya kuacha au kudai kuachwa.
MWISHO
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Maajabu ya wanawake
KWA uwezo na mapenzi yake Mwenyezi Mungu, tunakutana tena katika safu hii. Safu ambayo hutukumbusha tuliyoyasahau katika mahusiano yetu na kutufanya tumakinike nayo.
Hapa ninamaanisha, wifi kumchukia wifi yake; yaani dada kumchukia mke wa kaka yake na mke wa kaka naye kumchukia dada wa mumewe. Hatutaishia hapo, mama kumchukia mke wa mwanawe na mkwe naye kumchukia mama wa mumewe.
Niseme mapema tu kwamba, sio wanawake wote wenye tabia hizi, ni baadhi tu, ingawa ndio wengi.
Kinachofanya au kusababisha mafiwi na wakwe wasielewane ni kitendo cha wanawake wengi kutaka kuwatawala waume zao. Hiki ndicho chanzo cha mawifi, wakwe na wakati mwingine hata mashemeji kuchukiana.
Nitafafanua: Kwa kuwa wanawake wengi wana siri mioyoni mwao za kutaka kuwatawala waume zao hata kwa kutumia njia za kishirikina, basi kila mwanamke anamtazama mwanamke mwenzake kwa mtazamo huo.
Kwamba; dada anamtazama wifi yake kwa jicho la husda, akifikiri kaka yake anarogwa na mkewe ili atawaliwe, wakati mwingine hata kama hakuna matukio yanayoonyesha mwanamume ametawaliwa. Vivyo hivyo mama naye anafikiri mwanae anarogwa na mkewe.
Ni asilimia ndogo ya wanawake wasiyokwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta ‘dawa’ ya kuwadhibiti waume zao. Wanakwenda kutafuta dawa za kumfanya mwanamume afanye analotaka mwanamke. Wanamume wanalijua hili.
Hawaendi kwa waganga kutafuta dawa za kuimarisha mapenzi. Hawatafuti dawa za kujenga penzi lisitetereke wala kuimarisha uhusiano katika familia. Dawa zinazotafutwa ni dawa za kuwafanya wanaume wawe mazoba kwa wake zao.
Kwa kuwa yeye, (wifi au mama mkwe) ana tabia ya kwenda kwa waganga kumfanya mumewe awe ‘zezeta,’ na akubali kila anachokitaka. Ampangie matumizi na kumchagulia wa kumpa msaada na wakumnyima. Mume asahau kwao akumbuke ukweni, lazima naye atafikiri kaka yake au mwanawe anafanyiwa hivyo.
Hapa ndipo mahali pake ile methali ya Kiswahili isemayo “mkuki kwa nguruwe kwa binadamu uchungu.”
Ndio uchungu! Mama mkwe si anajua anachokifanya yeye na alichowafundisha watoto wake wakifanye kwa waume zao, basi anadhani na mtoto wake wa kiume anafanyiwa kama yeye anavyomfanyia baba yake.
Kila mtu anafahamu kwamba, majukumu baada ya ndoa yanaongezeka maradufu. Sasa mama mkwe na mawifi watataka wapewe huduma na kaka yao kama walivyokuwa wanazipata awali, wasipopewa watasema wifi yao anamzuia kaka yao .
Kwa upande mwingine aliyeolewa naye anaweza kuwa chanzo cha chuki na familia ya mumewe. Ameolewa akikuta falimia yenye utaratibu wake iliyojiwekea, yeye atataka kuubadirisha na kuleta utaratibu aliyotoka nao kwao.
Kabla ya kuolewa pengine alikuwa anajua kuwa mumewe ni mtu muhimu katika familia, baada ya kuingia yeye atataka kumtenganisha. Hapo lazima utatengeneza barabara ya chuki.
Mara nyingi tunaona wanawake wakiwapangia sheria waume zao; wanawachagulia watu wa kuwapa misaada, wakati mwingine mwamume anakatazwa hata kumsaidia mzazi wake na ikibidi wao (wanawake) ndio waidhinishe cha kutolewa.
Mwanamke wa aina hii anasahau asingempata mume aliyenaye kama si mama huyo anayemuona kero. Anajifanya kipofu wa akili kufahamu uwezo, usmati na pengine elimu aliyonayo mumewe imetokana na shida ilizopata familia yake kumtunza na kumsomesha.
Anasahau kama kuna siku na yeye atakuja kuwa mamamkwe. Anasahau kama yeye ana mama na kaka ambaye ameoa au atakuja kuoa na wala hataridhika akiona mama yake ananyanyaswa.
Wifi anafikiri kaka yake anatawaliwa – anamchukia wifi yake.
Mama anafikiri hivyo hivyo – anamchukia mkwewe.
Mke anazuia mumewe kusaidia ndugu zake – CHUKI TUPU.
NIPE MAONI YAKO!
USHAURI .....................?
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Vijana, ndoa na titi mchongoma
KUUANZA mwaka na kuumaliza si jambo dogo. Ni jambo linalohitaji rehema za Mwenyezi Mungu. Kutuchagua sisi wachache kuumaliza mwaka 2012 kati ya wengi tulioanza nao ni jambo la kushukuru.
Unapoingia tu mwaka mpya unapaswa kujiweka chini kutafakari mafanikio ya mwaka uliyopita kama yale uliyoyapanga umeyatekeleza ipasavyo.
Kwa kuwa safu hii tunayozungumzia zaidi masuala ya mahusiano ya kimapenzi na jamii kwa ujumla, leo babu yenu nimeona tuzungumzie vijana wa kiume waliopanga kuingia kwenye ndoa katika mwaka huu.
Kuna mambo mengi ya kuyafahamu na kuyazingatia kabla ya kuamua kuingia katika jukumu la ndoa ili usije ukajutia maamuzi yako. Kati ya mambo hayo mengi, leo nitawatajia mambo machache.
Upo tayari kwa ndoa?
Usikurupuke kuoa kama hujajipanga. Usioe kwa kuiga, wala kuoa kwa kutamani. Ndio, unaweza ukamtamani msichana na uwezekano wa kumpata kwa njia nyingine hakuna zaidi ya kumuoa. Ukaingia kwenye ndoa huku ukiwa bado hujajiandaa – ndoa hiyo haitadumu.
Vigezo vya mchumba
Oa kwa kuzingatia vigezo ulivyoweka vya mchumba unayemtaka. Usioe mwanamke usiyemridhia ukafikiri utajilazimisha kumpenda mkiwa kwenye ndoa, huta dumu naye.
Pamoja na kufuata vigezo ulivyoweka kwa mke unayetaka kumuoa, kuna mambo muhimu ya kuzingatia…
Ujue atachuja:
Umri wa miaka 15 mpaka 25 kwa wasichana wengi ndio umri wa ‘biashara.’ Katika umri huu wasichana wengi wanakuwa na mvuto – wanatamanisha wanaume.
Titi mchongoma litaporomoka
Wapo vijana wenzangu wanaovutiwa na matiti yaliyosimama mithili ya mchongoma. Kwa kawaida wasichana wengi wenye umri wa kuvunja ungo huwa na matiti mchongoma. Titi mchongoma ni kivutio kikubwa kwa wavulana wengi.
Tahadhari kwa kijana unayetamani kuoa msichana mdogo kwa kuvutiwa na titi mchongoma; ni muhimu kuelewa titi mchongoma halidumu. Wanawake wachache mno wanaoendelea kuwa na titi mchongoma wakiwa na umri mkubwa.
Idadi kubwa ya wasichana na wanawake titi mchongoma linaishia mwanamke anapozaa. Kwa hiyo, wewe kijana uliyepanga kuoa mwaka 2013, pamoja na kuweka kigezo cha kutaka titi mchongoma elewa titi hilo litaishia anapojifungua.
Kwa maana nyingine, mapenzi kwa mkeo yasiishe kwa kuporomoka titi, ingawa wakati unamuoa alikuwa na mchongoma. Hivyo ndivyo maumbile ya mwanamke yalivyo.
Wakati wa usichana anakuwa na titi mchongoma lakini kila umri unavyosonga na majukumu ya kifamilia yanapoongezeka titi linaporomoka.
Kiuno cha nyigu…
Kuna wale wanaopenda wasichana wembamba, wenye viuno vya ‘nyigu,’ bahati mbya wakiwaoa hawatambui kama shepu hiyo inahitaji matunzo maalumu ili kuifanya iendelee kuwepo.
Wanawake wengi wakishaolewa wanajiachia. ‘Dayati’ waliokuwa wnaifanya awali ili kubaki na miili ya kimisi huachana nayo. Hujiachia kwa kula ovyo na kuuachia mwili unenepe uwezavyo.
Wakati mwingine mwanamke akipata raha kwenye ndoa yake na akaridhika kunamfanya anenepe hata kama anafanya dayati.
Kuna umuhimu wa wakati huu wa mwanzo wa mwaka, vijana mnapopanga kupata wenza, kukumbuka kwamba, miili ya wasichana mnaotaka kuwaona haitaendelea kuwa hivyo.
Nimalizie kwa kusema kuwa; shepu za kimisi zinahitaji matunzo maalum. Titi mchongoma linategemea zaidi maumbile ya mwanamke. Msichana alivyo kabla ya kuzaa tofauti na atakavyokuwa akiwa na mtoto.
MWISHO
kaka uko vzuri sana ktk hz story na tips za mapenzi kwanini usiwe kama sultan tamba,musa banzi au shigongo? andika kitabu na utauza sikufichi
ReplyDelete