Gari la wagonjwa lililokuwa likimsafirisha hospitalini
rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela wiki mbili zilizopita,
liliharibika likiwa njiani kwenda hospitalini.
Msemaji wa rais wa Afrika Kusini Mac
Maharaj, amethibitisha kuwa gari hilo lilikumba na matatizo na kuwa ilibidi
rais huyo wa zamani kuhamishwa hadi gari lingine.
Hata hivyo Bwana Maharaj, amesema tukio
hilo halikuwa na tishio lolote kwa afya ya Bwana Mandela, kwa sababu alikuwa na
madaktari wa kutosha.
Shirika la habari la Marekani CBS
limenukuu vyanzo kadhaa vikidai kuwa Mandela alisalia katika eneo hilo kwa
zaidi ya dakika arubaini kabla ya usaidizi kufika.
Shirika hilo la CBS limesema kuwa wakati
Bwana Mandela alipokuwa akihamishwa hadi gari lingine viwango vya joto vilikuwa
chini sana.
Mandela, mwenye umri wa miaka 94,
alikuwa akisafirishwa kutoka hospitali moja mjini Johannesburg hadi Pretoria,
wakati wa tukio hilo lililotokea tarehe nane Juni mwaka huu.
Mandela alilazwa hospitalini huku hali
yake ikiwa mbaya kutokana na maambukizi ya mapafu ya mara kwa mara na tangu
wakati huo amekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Hii ni mara ya tatu kwa Bwana Mandela
kulazwa hospitalini mwaka huu
Kutoka BBC
0 maoni:
Post a Comment