
Wanawake wawili wameambia gazeti la New York Times kwamba mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump aliwashika kimapenzi bila idhini yao.
Mwanamke mmoja amesema mgombea huyo alimshika matiti na kujaribu kuingia mkono wake chini ya sketi yake wakiwa kwenye ndege miongo mitatu iliyopita.
Wa pili anasema Bw Trump alimpiga busu bila yeye kutaka katika jumba la Trump Towers mwaka 2005.
Maafisa wa kampeni wa Trump wamesema "makala hii yote ni hadithi ya kubuni".
Gazeti la New York Times limeanzisha kampeni "ya uongo, na iliyoratibiwa kumharibia jina kabisa", taarifa ya maafisa wa Trump imesema.
Jessica Leeds, 74, kutoka Manhattan, ameambia gazeti hilo kwamba alikuwa ameketi karibu na Bw Trump sehemu ya abiria wa hadhi ya juu kwenye ndege wakielekea New York pale alipoinua sehemu ya kupumzishia mkono kitini na akaanza kumshika.
Mwanamke huyo alikuwa na umri wa miaka 38 wakati huo.
"Alikuwa kama pweza .... mikono yake ilinishika kila pahali," anasema. "Ulikuwa ni unyanyasaji."
Kutoka BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment