Shinikizo zaidi dhidi ya rais Morsi
Rais wa Misri Mohammed Mosri anaendelea kukabiliwa na shinikizo kali huku maafisa zaidi wa serikali yake wakiendelea kujiuzulu nao waandamanaji wakianza kukusanyika tena katika bustani ya Tahrir.
Msemaji wa rais na mwenzake wa baraza la mawaziri nao pia wamejiuzulu , baada ya mawaziri sita kuondoka serikali mwishoni mwa wiki kufuatia maandamano makubwa dhidi ya serikali.
Awali taarifa ya rais ilipinga vikali onyo la jeshi dhidi ya utawala wa Morsi kwa kumpa masaa 48 kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaokumba taifa hilo.
Chama rasmi cha upinzani National Salvation Front, kimesema kinaunga mkono tamko la jeshi lakini katu hakiungi mkono mapinduzi ya kijeshi.
Taarifa hiyo ya rais imesema kuwa hatua hiyo ya jeshi kuingilia kati itazua hali ya suitofahamu zaidi.
Jeshi limekanusha madai kuwa makataa hayo ni sawa mapinduzi ya kijeshi.
Serikali imesema kuwa Morsi amewasiliana na rais Barack Obama kuhusu hali ya kisiasa inayoshuhudiwa Misri.
Wakati huohuo, shirika la habari la kitaifa Misri, limeripoti kuwa waziri wa mambo ya nje Mohamed Kamel Amr amejiuzulu.
Ikiwa ombi lake litakubaliwa, atakuwa mmoja wa mawaziri wengine watano ambao wamejiuzulu kufuatia mgogoro huo wa kisiasa.
Mnamo jumapili, mamilioni walifanya maandamano wakimtaka rais ajiuzulu.
Maandamano mengine makubwa yalishuhudiwa Jumatatu huku ripoti zikisema kuwa watu wanane waliuawa wakati waandamanaji walipovamia makao makuu ya chama tawala cha Muslim Brotherhood.
Wapinzani wa Morsi,wanamkosoa kwa kuweka maslahi ya chama mbele huku akiwapuuza wale wasiounga chama hicho.
Morsi alichaguliwa kama rais wa kwanza wa kiisilamu katika uchaguzi wa mwezi Juni mwaka 2012 tarehe 30 baada ya kushinda uchaguzi uliotazamiwa na wengi kuwa huru na wa haki baada ya mapinduzi ya kiraia yaliyomwondoa mamlakani Hosni Mubarak
kutoka, BBC
0 maoni:
Post a Comment