Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima
la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo
kuvamiwa na wanamgambo.
Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya
jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea
kukamilisha operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa
wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.
Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya
170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.
Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka
jengo zima la Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba
hakuna mateka aliyesalia
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati
ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na
mwanamke muingereza.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini
Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka
18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota.
Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa
amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.
Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani
waliko.
Haijulikani idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani ya jengo hilo ,
lakini maafisa wa usalama wamesema kuwa wanamgambo watatu wameuawa.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo,
kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.
Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa
waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.
"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu
mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na
majeshi,'' alisema Ole Lenku
Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.
Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye
jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na
wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka
kukomboa jengo hilo.
Kutoka BBC.
0 maoni:
Post a Comment