Shirika la afya duniani WHO,
linasema kuwa mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa Ebola hautarajiwi kushuhudiwa
katika mataifa Ulaya kwani nchi za Magharibi zina mifumo thabiti ya
afya kuweza kukabili ugonjwa huo..............
Rais Barack Obama wa Marekani pia amesema hatari kwa Wamarekani kupata virusi vya Ebola ni ya "chini mno", ingawaje ameagiza"hatua thabiti zichukuliwe" kukabiliana na ugonjwa huo.
Marekani inachunguza namna mtu aliyeambukizwa Ebola alivyoruhusiwa kusafiri kwenye ndege na kumwambukiza muuguzi aliyekuwa akimtibu huko Texas.
Maafisa wanajaribu kufuatilia watu 132 waliosafiri na Amber Vinson.
Ugonjwa huo umeua watu wapatao 4,500 mpaka sasa, hususan katika nchi za Liberia, Guinea na Sierra Leone.
Mawaziri wa Afya wa Umoja wa Ulaya watakutana mjini Brussels Alhamisi kujadili janga hili, ikiwemo uwezekano wa kupeleka askari zaidi huko Afrika Magharibi kusaidia kudhibiti ugonjwa huo.
Mkurugenzi wa mkakati wa WHO, Christopher Dye, amesema kulipuka kwa Ebola nchini Marekani au nchi nyingine Ulaya Magharibi ni jambo ambalo limeleta "wasiwasi mkubwa"
"Uwezekano kwamba mara maambukizo yakitokea yanasambaa kwingineko, ni jambo ambalo kila mtu atakuwa na wasiwasi nalo, amesema.
Lakini ameongeza kusema: "lakini tuna uhakika kuwa Amerika Kaskazini na Ulaya magharibi ambako mifumo ya afya ni imara sana, kwamba hatutarajii kuona mlipuko mkubwa katika moja ya maeneo hayo."
Mapema, Rais Obama alisema uwezekano wa kusambaa kwa Ebola kwa kiasi hicho kama cha nchi za Afrika magharibi ni "mdogo sana sana."
Hata hivyo, ameahidi "hatua thabiti zaidi" katika kufuatilia wagonjwa wa Ebola nchini Marekani na amethibitisha mipango ya kupeleka"timu mkakati" ya wataalam katika hospitali yoyote ambayo imeripoti maambukizo ya Ebola.
Kutoka BBC"
0 maoni:
Post a Comment