MWERA AMAZING BLOG

MWERA AMAZING BLOG
                                      LULU KIZIMBANI KWA MAUWAJI YA KANUMBA   
              

  Na mwandishi                   
MSANII wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka ya mauaji ya msanii mwenzake anaye daiwa kuwa alikuwa mpezi wake, Steven Kanumba.

Lulu aliletwa mahakamani hapo jana saa tano asubuhi kwa siri huku akiwa chini ya uangalizi wa askari kanzu sita; wanawake wawili huku wakimficha asionekane na watu na waandishi wa habari waliokuwepo mahakamani hapo wakimsubiri baada ya kupata fununu za kwamba angepandishwa kizimbani .

Baada ya kusimamishwa mbele ya Hakimu Agustino Mmbando, Mwendesha Mashitaka, Wakili Mkuu wa Serikali, Beatrice Kaganda alidai kuwa Lulu ambaye ni mkazi wa Tabata ana umri wa miaka 18. Hata hivyo, Lulu alikanusha umri huo mbele ya Hakimu Mmbando na kudai kuwa ana miaka 17.

Kaganda aliendelea kumsomea mashitaka yanayomkabili ambapo alidai Aprili 7, mwaka huu eneo la Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, alimuua mtu aliyejulikana kwa jina la Steven Kanumba.

Lulu hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji na hivyo kesi hiyo kupangiwa kutajwa Aprili 23, mwaka huu mahakamani hapo.

Atolewa chapchap Kama alivyoingizwa mahakamani hapo, Lulu aliyekuwa amevaa vazi maarufu kwa jina la dera la rangi ya njano na kujifunika kwa mtandio wa rangi ya pinki kichwani mpaka usoni ili asionekane, alitolewa kwa haraka.

Wakati akitoka kupitia mlango wa nyuma, mshitakiwa huyo pamoja na askari kanzu waliokuwa wakimlinda, walikuwa wakikimbia huku wakimficha na kumuingiza kwenye gari iliyokuwa na vioo vya giza ambalo liligeuza na kuondolewa kwa haraka.

Gari hilo Suzuki Grand Vitara nyeupe yenye nambari za kiraia T848 BNV na kwenye kioo ilikuwa na namba tofauti ambayo ni PT 2565 ambapo alidaiwa kupelekwa Gereza la Segerea.

Hali hiyo, haikuwapendeza waandishi wa habari ambao walikuwa mahakamani hapo tangu asubuhi kusubiri kesi hiyo ambayo walikuwa na fununu kuwa angepelekwa Kisutu, wengine wakidai kuwa walielezwa na Polisi kuwa msanii huyo angepelekwa Mahakama ya Kinondoni.

Kanumba (28), aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, alifariki usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza Vatican, baada ya kudaiwa kutokea ugomvi kati yake na Lulu anayedaiwa alikuwa mpenzi wake.

Alizikwa juzi katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam. Utabiri kifo cha Kanumba Kampuni ya maigizo aliyokuwa anamiliki msanii huyo mahiri ya Kanumba The Great Film Production, inasubiri idhini ya familia ya msanii huyo kabla ya kusambaza filamu zake mpya, ikiwemo aliyoigiza kisa chenye matukio yanayodaiwa kuwepo katika kifo chake.

Mpigapicha Mkuu wa Kanumba, Zakayo Magulu alisema jana kuwa Kanumba aliacha filamu mpya mbili ambazo hazijaingia sokoni; Ndoa Yangu na Power and Love aliyoigiza anakufa baada ya kusukumwa na mkewe.

Magulu alisema filamu ya Power and Love imeshakamilika na siku moja kabla ya kufariki, alikuwa anatakiwa kuipeleka kwa Kampuni ya usambazaji ya Steps Entertainment aliyokuwa akiitumia kusambazia filamu zake.

Akiizungumzia filamu hiyo, Magulu alisema Kanumba ni kama alijitabiria kifo chake kwa kuwa sehemu kubwa inaendana na kifo chake.

Filamu hiyo kwa mujibu wa Magulu, ni yake ya kwanza kuigiza kuwa anakufa na kifo chenyewe kinasababishwa na kusukumwa na msichana aitwaye Irene Paul.

Alisema pia katika filamu hiyo, Kanumba anaigiza kuwa baada ya kusukumwa, anaanguka chini na anakuja daktari wake aitwaye Pancrase ambaye ndiye daktari huyo huyo aliyefika kumwangalia mara baada ya kuanguka siku ya kifo chake.

Pia alisema katika filamu hiyo kulikuwa na mwigizaji mwenzake aitwaye Kupa, ambaye anaigiza kuwa mtu wa mwisho kumuona kabla ya kuingizwa chumba cha maiti, ambaye wakati wa kifo chake ndio hivyo hivyo kwani Kupa ndiye alikuwa wa mwisho kumuona siku hiyo.

“Mimi naona kuwa huyu bosi wetu, ndugu yetu ndio alikuwa anajitabiria kifo chake hasa haya mazingira ya kisanii katika filamu na ndio imekuwa hivyo hivyo katika hali halisi, filamu hii ikitoka haya yote yataonekana,” alisema Magulu.

Filamu hiyo inahusu msaada wa figo ambao Kanumba anautoa kwa Irene kwa lengo la kumshawishi awe mpenzi wake, lakini baadaye Irene anarudi kwa mwanamume wake wa zamani.

Magalu alisema kuwa katika filamu hiyo Kanumba, anaigiza kukasirishwa na kitendo hicho na baadaye anagombana naye na msichana huyo anamsukuma ndipo anakufa. Akizungumzia filamu ya Ndoa Yangu, alisema kwa sasa ipo katika hatua ya uhariri na imekamilika kwa asilimia 60 ambapo filamu hiyo Kanumba ameigiza akiwa na Jacquline Wolper.

Alisema filamu hiyo inagusia maisha ya ndoa ya Kanumba ambapo ameigiza kuwa alikuwa na mke aliyekuwa na ujauzito uliokuja kutoka baadaye na Kanumba kujikuta akiwa hana hamu ya tendo la ndoa na mwanamke huyo, na kutembea nje mpaka alipokuja kufumaniwa. Alisema filamu hiyo ipo sehemu ya kwanza na ya pili huku ile ya Power and Love ikiwa ni moja tu. Mauzo lini?

Alisema kwa kawaida Kanumba alikuwa na utaratibu wa kujadiliana na wafanyakazi wake hao kabla ya kuamua siku ya kuuza masta ya kazi ambayo wameirekodi.

Alifafanua kuwa wao kama wafanyakazi hawawezi kuipa haki kampuni hiyo kusambaza kazi za Kanumba mpaka familia yake iseme ndio wafanye hivyo na ndio taratibu za kusambaza zianze. Imeandikwa na Evance Ng’ingo na Regina Kumba
        NA mweraamazing.blogspot.com
Share on Google Plus

About MWERA AMAZING

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

1 maoni: