MAPENZI NI KUPENDANA NA SI KUTESANA |
HALI ya mambo katika uhusiano wako ikoje? Wewe mwenyewe unalo jibu, lakini kwa vyovyote itakavyokuwa ni muhimu kufahamu kuwa kutesa familia, eti kisa una mtu nje, huchangia kuleta laana katika maisha ya mwanadamu. Huenda ikawa ndoa yako ni nzuri, ya kuridhisha kidogo au huenda ni mbaya hadi umeanza kujuta kwanini ulikutana na huyo mtu ambaye unaye sasa. Zamani mlikuwa mna kawaida ya kutembea pamoja na mwenzi wako, lakini sasa anakuona haufai tena kutembea naye? Je mara ya mwisho ni lini ulikuwa pamoja katika matembezi na mkeo au mumeo? Kuna watu akili zao zimeharibika; anaona mke au mumewe hana maana tena, wenye maana kwake ni wapenzi wan je. Wenye akili timamu, huangalia namna ya kuimarisha ndoa zao,sio kukimbilia wapenzi wa nje. Ni ujinga kwa mfano kutelekeza familia na kukimbilia wanawake wengine…watakusaidia nini ndugu yangu au ukinalihii unatoa dhahabu!! Ni akili isiyo na maana, hata kama iwe hivyo. Ni muhimu kuheshimu familia, ni muhimu kuwajali watoto. Ujana maji ya moto ndugu yangu, uzee unakuja, ni ngumu kutarajia mazuri kutoka nyumba ndogo au wanaume wa nje. Ni makosa kutegemea kuvuna mpunga, wakati sasa unayopanda shambani mwako ni bangi. Fanya mema, kwa kuishi vizuri na familia yako, kwa kuwajali watoto wako na kupanga mikakati mizuri ya maendeleo. Dalili kwamba huna akili ni kuwasaidia wanawake wa nje ya ndoa kama vile kuwasomesha, kuwanunua magari na mambo mengine, badala ya kusaidia nyumba na familia yako iwe imara, kiasi kwamba hata kesho na keshokutwa ukiumwa au kutokuwa na uwezo, wawe na nguvu za kukusaidia. Ndugu yangu jitahidi kuwa na ‘akili’…bila shaka tumeona wengi wakipooza miili, tumeona wengi wakifilisika na mambo mengine kama haya, ni muhimu kuangalia namna ya kufanya ili kuhakikisha nawe unakuwa na hatma nzuri hata pale Mungu atakapokufikisha kwenye uzee nk. Kuna watu wengi wanapozeeka wanakuwa kero kwa familia zao, eeeh mbona hamnisaidii…aaah mnakula tu wenyewe…ndivyo baadhi ya wazazi wanavyolalamikia watoto wao, swali la kujiuliza hapa ni je wakati wa ujana wako kuna mambo yapi ulikuwa ukiyafanya? Watu wengine leo wanalalamika, lakini wanasahau kuwa walichangia kufanya ujinga katika maisha yao, ni vizuri ndugu yangu kutafakari kwa makini ninachokueleza. Wengine wanaringa, eti wanaringia vyeo vya kuajiriwa….ndugu yangu dalili kwamba huna akili timamu ni kuringa kwa kuwa ni bosi sehemu fulani. Mwenye akili haringii vyeo vya kuajiriwa bwana….ajira ni suala la muda tu, mikataba mingi inasema kwa mfano ukiumwa miezi sita, kazi basi, lakini pia inasema ukifika umri fulani kazi basi. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba mwenye akili, anapokuwa na fedha, anazitumia kama mtaji kuanzisha miradi yake iwe imara…tafiti nyingi zinaonyesha kuwa watu ambao wanaishi kwa kutegemea ajira kwa asilimia mia, hatma yao ya kimaisha huishia kubaya…wengine huishia hadi kuwa ombaomba. Wenye kupaswa kuringa angalau ni wale ambao wamejianzisha miradi yao hata kama ni midogo, maana ni ukweli kwamba akiumwa, fedha zinaweza kuendelea kusaidia kuendesha biashara yake. Ni ujinga, leo una fedha unamuona mpenzi wako hana maana tena, unamtafuta mwingine mpya, ambaye hasa anakupenda kwa sababu ya kutamani zaidi kukuchuna. Ni vizuri kuendelea kumpenda mtu ambaye umetoka naye mbali, mtu ambaye amekuwa ni msaada katika maisha yako. Aliyekuvusha katika hatua fulani kimaisha, ndiye anayepaswa kuendelea kuheshimiwa, hata kama labda ana mapungufu, ni vizuri kuangalia namna ya kuondoa kasoro hizo, kwa sababu ni ukweli kuwa hakuna mtu ambaye yuko sahihi au hana kasoro kwa asilimia mia. Ni vizuri kuangalia historia za watu, je baba au babu yako, ndoa yake waliishi kwa amani na maelewano tu kwa asilimia mia? Jibu lake, sio. Hata uoane na nani, kasoro ndogo ndogo zipo, tatizo kubwa ni kwamba kuna wengine, jambo dogo kwake linakuwa kubwa, wengine wanasema nimekusamehe, halafu kesho mkigombana, anakumbushia namna juzi mlivyogombana, kitu ambacho sio sahihi hata kidogo. Maisha yetu yanatuhitaji kusamehe na kusahau. Utaweka visasi hadi lini ndugu yangu? Ni vizuri kuangalia mbele, achana na mambo ambayo yanakuumiza moyo, angalia namna ya kupata furaha katika maisha yako. Ndugu yangu ‘vizuri vina kasoro, vibaya hujitembeza’ ndio msemo mpya ambao unapaswa kuuelewa. Hata mume au mke, kwa haraka unaweza kumuona mzuri, ni sawa, lakini kasoro za hapa na pale lazima zitakuwepo. Hata wale wanaoelezwa kuwa wabaya, tunaambiwa kuwa hujitambezwa…ni imani ya watu na misemo yetu ya Kiswahili, ninachotaka kusisitiza ni kwamba ni muhimu kuwa makini unapofikiria kuwa na mwenzi. Na unapokuwa na mwenzi, ni vizuri kuangalia namna ya kufanya ili aweze kuwa nawe katika hali ambayo haitakuletea majonzi. KASORO NI NYINGI: Katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti, kwa maana ya vipindi vizuri na vibaya. BUNI MAMBO MAPYA ILI MWENZI WAKO ASIKUCHOKE; Katika maisha ya ndoa, ni suala la msingi kuangalia namna ya kufanya ili kuhakikisha mnakuwa na ndoa nzuri. Ni vizuri kwa mfano kujuana kwa kina tabia na kuangalia nini cha kufanya ili muweze kuendana katika hali ambayo itamfanya kila mmoja wenu kuendelea kuwa na amani katika ndoa yake. Msingi wa kuendelea kuishi kwa amani, ni pamoja na kuruhusu majadiliano katika ndoa. Kwamba kama kuna tatizo fulani, kaeni chini haraka na kuangalia nini cha kufanya ili kuondoa kasoro iliyopo. Ni vizuri kila upande kufahamu nini hasa majukumu yake katika ndoa. Ni aibu kwa mfano mume kutowajibika kwa mkewe, eti kwa kisingizio kuwa labda mke naye anafanya kazi nk. Katika maisha ya ndoa, mume anapaswa kuendelea na majukumu kama vile kununua mavazi ya mkewe nk, lakini inasikitisha sana kuona baadhi ya wanaume, hawajui wake zao wamevaa nini, hadi nguo za ndani za wake zao wanajinunulia wenyewe, kitu ambacho sio sahihi. Raha ya nguo za ndani kwa mfano ununuliwe na mwenzi wako, eeeh ndugu yangu. Kama mwenzi wako afanye hivyo, ni suala la kuzungumza na kukumbushana, kwamba huu mwili ni wako, unapaswa kuujali na kuangalia unakuwaje. Kufanyiana vitu kama hivi husaidia kuimarisha uhusiano, kwa maana mtu atajiona anajaliwa. ...................................... NI MUHIMU SANA: Katika siku zote za uhusiano wenu kutamka na kuangalia namna gani mnaimarisha uhusiano wenu. Tamka maneno ya kuonyesha ni kwa namna gani unampenda mwenzi wako, au ni namna gani mwenzi wako ni muhimu katika uhusiano wenu. Katika mapenzi, kuna maneno ya kutilia maanani kama vile ‘nakupenda sana mpenzi wangu, nafurahi kuwa nawe, namshukuru Mungu aliyenikutanisha nawe’ nk. Je unafikiri ni sahihi Mungu kukutanisha na mke au mume ambaye unaye sasa? Sijui una jibu gani, kwa vyovyote itakavyokuwa, ni suala la msingi kwa wanandoa kuombeana mambo mazuri na kusaidiana ili waweze kuwa na maelewano mazuri. Kama niliyotangulia kusema, matatizo tumeumbiwa wanadamu, kama ni kukwaruzana, hata mama yako kuna wakati mnakosana, licha ya kwamba ulikaa tumboni mwake, iwe mtu ambaye mmekutana tu mitaani? Ni vizuri kuangalia namna ya kusaka amani na mwenzi, badala ya kufikiria kuachana na kutafuta mwingine. Kama ambavyo huyu wa sasa mlianza katika mapenzi motomoto, na sasa mnakwaruzana, ndivyo ambavyo inaweza kutokea kwa huyo mpenzi mpya ambaye unamfikiria kuwa ni mzuri sana na kumdharau mtu ambaye unaye sasa. Kama unataka kuishi maisha ya shida, telekeza familia au mtesa mkeo, kwa sababu labda sasa una nyumba ndogo!! Mume au mke kumwambia mwenzake NAKUPENDA kuna maana nzuri katika nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama. Neno hili huzidisha maelewano na kustawisha mapenzi. Haifurahishi hata kidogo, wakati mwingine unaweza kumwambia mtu ‘Nakupenda’, halafu anakujibu ‘haya’ au “Acha utani, sisi tumeishazeeka”. Hata muwe wazee, bado mnapaswa kuendelea kuonyesha kupendana, kwani ndio msingi wa kuwafanya muendelee kuwa na amani na afya njema zaidi. Kwa wanawake wazee sio tatizo sana, ila kwa wanaume wazee, wapo ambao bado wanapenda kuendeleza ngono hasa na mabinti na kwa ujumla kuna kundi kubwa la watu wenye umri mkubwa, wanapenda kuwa na mabinti au kuendelea kupendwa katika suala zima la mapenzi. Kwa ujumla mapenzi, kwa wanaume ni suala lisilo la ukomo, wanapenda kuelewa kupendwa hadi wanapokuwa wazee na kukongoroka kabisa. Kwao mapenzi ni jambo la msingi hasa suala zima la mahaba, wakati kwa wanawake, sio sana, ingawa kama wanapata wanaowaheshimu huwa na amani na furaha zaidi. LINI ULIMPELEKEA ZAWADI MWENZI WAKO? Zawadi ni njia nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako na nafasi ya mwenzako katika maisha yako. Lakini ni muhimu kuacha kuongea maneno mengine yasiyo na ulazima wakati wa utoaji wa zawadi…maana kuna wengine wanatoa zawadi huku anaongeza kusema ‘mimi nakupa lakini wewe huwa hunipi zawadi, sijui unaona kama najikomba au vipi?’ Ndugu zangu peaneni zawadi mtapendana zaidi. Aidha katika kupeana zawadi ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda mwingine ili zawadi iwe na maana zaidi kwa yule anayepewa, na iwe ni zawadi maalum kwa mlengwa, isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo, kwa mfano, si vema kwa mwanamme kumletea mkewe zawadi ya sufuria nk hiyo haitaitwa zawadi. Lakini zaweza kuwa manukato ayapendayo, hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu, na vitu ambavyo ni maalumu kwa matumizi yake binafsi. Hali kadhalika kwa mwanamke kumzawadia mumewe achunge vigezo hivyo, hii ndio huwa hasa maana ya zawadi. BADIRINI MAZINGIRA; Kubadili mazingira ni suala la msingi sana katika maisha, kwa mfano mmoja anaweza kumuomba mwenyewe kwamba leo wakale chakula sehemu fulani mbali na nyumbani. Sijui ni lini ulimwambie mumeo au mkeo hilo, ila ni vizuri siku moja kumwambia mwenzi wako katika hali ya kushtukiza kwamba labda naomba twendwe sehemu fulani nje ya nyumbani kwa lengo labda la kula chakula cha usiku na mambo mengine kama haya. Maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja kila siku humfanya mtu kuyachoka, ni vema wanandoa na hasa wanamke kuwa wabunifu kwa kubuni vitu vitakavyotia radha mpya katika nyumba, ikiwemo hiyo njia niliyoieleza hapo juu. Hali kadhalika mwanamume naye anaweza kumualika mkewe katika hoteli ya heshima mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya kujikumbusha mambo mazuri yaliyopita. Je utajisikiaje, siku mkeo au mumeo atakapokutoa ‘out’ kwa chakula au mambo mengine yanayofanana na hayo? Bila shaka ni tamu.Ni makosa kupeleka hoteli za heshimu wapenzi wa nje au kwenda kwenye hoteli za heshima wakati wa mikutano tu. Sio lazima mnapokwenda hoteli ya heshima mle chakula maana ni ghari, mnaweza kwenda japo kununua soda tu na maji au juisi ambayo hata sh10,000 haitaisha. Pia sio lazima kwenda kila siku, kuna siku maalum mnaweza kuchagua. Jambo hili husaidia kunogesha mapenzi, kuna wengine watatangaza hadi mtaani mume wangu kanipeleka hoteli nzuri ambayo sikuwahi kupelekwa na mtu yeyote katika maisha yangu…hili ni jambo zuri na huonyesha mnajaliana. Je wewe ukoje? Tafakari, chukua hatua kuimarisha ndoa yako. IFANYE NYUMBA KUWA NA MVUTO; Mke mwerevu huwa anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba, kwani mazingira ya nyumba yanapokuwa ni yale yale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu, kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa basi rangi ni zilezile, hali hii humfukuza mwanamume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala tu, na huu ndio mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba. Ndio unaweza kuona wanaume wengine wanarudi nyumbani usiku wa manani hata kama hana kazi maalum za kufanya kwa sababu tu nyumbani hakuna mvuto, kuna kelele au labda hakuna chochote cha kumvutia. Wanawake wengine hawana muda wa kukaa na waume zao, akiwa nyumbani anajifanya yuko bize hata kama hayuko bize kweli. KUOGA HADI UAMBIWE; Kuna watu wengine wako kwenye ndoa wamekuwa wachafu, hata kuoga hawaoni kama ni jambo muhimu kwao. Baadhi ya watu hasa wanawake hufikiri kwamba hata kama hajaoga, akipata losheni ni usafi, sio kweli, ukipata losheni au mafuta kwenye uchafu, harufu yake inakuwa mbaya zaidi. Ninachotaka kuzungumzia hapa ni umuhimu wa wanandoa kuwa wasafi. Angalau wanawake, ila kuna wanaume wengi ambao wanakwenda kulala vila kuoga. Kuna wengine wananuka, lakini wapo wenzi ambao huona ni vizuri kuendelea kubaki kimya. Wanaume nao hudhani kuwa kwao wanaume ndio wamepewa kibali cha kuwa wachafu, kwa mfano wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho, na wengine wana matatizo sugu ya kunuka miguu, huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi. Wengine kuoga usiku ni suala lisilokuwepo kwa nafsi zao. Hii sio sahihi hata kidogo. Aidha baadhi ya wanaume hawana uchaguzi sahihi au hali ya kuvutia katika uvaaji, kiasi kwamba kwa baadhi ya wanawake huona haya hata kuwatambulisha mbele za jamaa zao au kutembea nao. Ni vizuri katika maisha ya ndoa, kuvaa kitu ambacho mwenzi wako anaweza kukifurahia. ISHI KWA KUTEGEMEA DINI YENU MNAYOIAMINI; Wewe ni mtu wa dini au dhehebu gani? Au ni mtu mwenye kuamini nini? Ni suala la msingi katika maisha ya ndoa kuishi kwa staili ya imani yako ili kuyafanya maisha yako kuwa ya maana zaidi. Wanandoa wanapaswa wakati fulani kutembelea vituo vya kulelea yatima, kuwa na mpango fulani wa kusaidia wasiojiweza na mambo mengine kama haya ambayo kimsingi husaidia kuongeza baraka katika maisha yao na kufikia kasoro zao. Ni muhimu pia kutembelea wagonjwa, ndugu na jamaa wengine katika maisha. Kiimani, kusaidia wahitaji kama watoto yatima, wajane na kusali ni kati ya vitu vinavyosaidia kuharakisha maendeleo kwa mtu. |
0 maoni:
Post a Comment