MWERA AMAZING BLOG

MWERA AMAZING BLOG

SHIRIKA la kuhudumia watu wenye ulemavu wa ngozi,
 (Under The Same Sun -UTSS) limeitaka Serikali na
 viongozi wa kisiasa kurejesha amri ya kupiga marufuku
 shughuli zote za waganga wa jadi na wa tiba asilia ili
 kukomesha matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu huo.

Hatua hiyo imekuja kutokana na  mauaji ya
 mwanaume mmoja asiyetambuliwa jina mwenye
 umri kati ya miaka 25 hadi 35 ambaye mwili
 wake kukutwa umenyofolewa viungo mbalimbali
 kama vile sehemu ya makalio, sehemu yote ya nyeti zake,
 nywele za kichwani, ulimi, ngozi ya usoni, mikono yote,
 masikio na koromeo.

 Akizungumza na waandishi wa habari jijini
 Dar es Salaam jana, Afisa Utetezi kutoka katika
 shirika hilo, Kondo Seif, alisema mwili wa mwanaume huyo uligunduliwa Mei 26 mwaka huu katika kijiji cha Nambala, kata ya Kikwe, tarafa ya Mbughuni, wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Alisema mauaji ya mwanaume huyo yanasadikiwa kuwa yalitokea kati ya Mei 19 hadi 22 mwaka huu kwani tayari mwili huo ulikuwa umeshaanza kuharibika vibaya.

“Inasadikiwa mwili wake ulikaa hapo kwa muda wa wiki moja, kwa sababu wakazi wanaoshi maeneo hayo walianza kusikia harufu kali kwa siku kadhaa ndipo wakaamua kutafuta chanzo chake na kuukuta mwili wake umelazwa kufudifudi juu ya jiwe kando ya mto Nambala kilomita 40 kutoka Mererani.

“Unyama huu umekithiri kiasi kwamba wauaji hata hawakuusitiri mwili wake baada ya kukata viungo mbalimbali kwani ulikuwa mtupu na suruali yake ilikuwa imevuliwa hadi kwenye vifundo vya miguu.

“Lakini cha kushangaza ingawa mwili wake hadi sasa umehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru, hakuna ndugu hata mmoja aliyejitokeza kudai kama kuna ndugu yake amepotea.

“T-shirt ya rangi ya bluu iliyoiva ilikutwa karibu na mwili huo pamoja na sahani nyeupe ya udongo, hivyo UTSS inatoa wito kwa Watanzania wenye ndugu, jamaa  na marafiki wenye Albinism kama wamepotelewa na mpendwa wao,” alisema.

Aidha alisema katika kipindi kifupi cha miezi mitatu iliyopita kumetokea matukio sita ambayo mawili ni vifo na matatu ni majaribio ya mauaji na moja na utekaji nyara.

“Hali hii inaashiria kwamba, wimbi la mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na ukataji wa viungo nchini bado linaendelea na juhudi za makusudi zinahitaji kukabiliana na tatizo hili.

“Tukio la jingine ni la kutekwa nyara kwa mtoto wa kiume  mwenye albinism anayedhaniwa kuwa ametokea Tanzania ambapo mtoto huyo mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka mitatu alionekana uwanja wa ndege wa kimataifa wa Nairobi nchini Kenya akisafirishwa kutoka Tanzania na watu watatu wenye asili ya Kiafrika wanaozungumza Kifaransa wakielekea Burkina Faso,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo watu wengi wamekuwa wanaendelea kuwa na dhana kuwa albino huwa hafariki na badala yake hupotea jambo ambalo si kweli.

“Dhana hii imeendelea kusababisha mauaji hayo yaendelee kutokea kwa sababu hata huyu mwanaume aliyeuawa bado hajafahamika, ina maana wanachukulia kama amepotea.

“Ndio maana tunaitaka Serikali na hata Wabunge wetu, wapige kelele huko bungeni kukomesha kabisa shughuli za hao waganga wa kienyeji.

“Kama kweli hawaamini ushirikina, uchawi na hawaamini na kuwatumia waganga wa kienyeji warejeshe amri ya kupiga marufuku shughuli za waganga hao,” alisema.
MWISHO

Share on Google Plus

About MWERA AMAZING

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 maoni:

Post a Comment