MNYIKA
ALILIA AHADI YA JK
MBUNGE wa Ubungo John Mnyika, (CHADEMA) amesema
ofisi yake haijaridhika na majibu yaliyotolewa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuhusu ahadi ya Rais Jakaya
Kikwete ya kukutana na mamlaka zinazohusika huduma ya maji katika Jiji la Dar es
Salaam badala yake inasubiri barua rasmi kutoka Ikulu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Machi 20 mwaka huu
Rais Kikwete wakati akizindua daraja la Golani katika Kata ya Kimara, kuahidi kuwa
ifikapo Machi 25 atakukutana Ikulu, pamoja na watendaji wa mamlaka zinazohusika
na sekta ya maji sambamba na wabunge mkoa wa Dar es Salaam kujadili hatma ya
upatikana wa huduma ya maji.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa jana na Katibu Msaidizi wa Mbunge huyo, Aziz Himbuka kwa niaba
yake, alisema Rais Kikwete aliahidi angekutana mwezi mmoja kabla ya
kuwasilishwa bungeni kwa bajeti ya Wizara ya Maji hali ambayo hadi sasa
haijatekelezwa.
Alisema kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, Hotuba
ya Bajeti ya Wizara ya Maji kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara
hiyo ikiwemo kuhusu miradi ya maendeleo katika sekta ya maji itawasilishwa
bungeni tarehe 24 Aprili na kuhitimishwa tarehe 25 Aprili 2013.
“Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inatoa mwito
kwa Ofisi ya Rais kutoa ufafanuzi kwa umma iwapo mkutano huo utafanyika kabla
ya kusomwa au kuhitimishwa kwa bajeti ya Wizara ya Maji na iwapo mkutano huo
utafanyika baada ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, Ofisi ya Rais
itahakikisha vipi hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na
ushughulikiaji wa maji taka katika jiji la Dar es Salaam.
“Ofisi ya Mbunge imelazimika kutoa taarifa hii kwa
kuwa tangu Machi 26 2013 wananchi kutoka
maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo na jiji
la Dar es Salaam wanaulizia matokeo ya mkutano huo baadhi kwa kufika ofisini na
wengine kuulizia kwa njia mbalimbali za mawasiliano; hivyo ofisi ya Rais
ilichukulie suala hili kuwa ni lenye maslahi kwa umma,” alisema.
MWISHO
0 maoni:
Post a Comment