Mgonjwa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Naivasha |
Wananchi wa Kenya
wameshangazwa na taarifa ya mwanamume mmoja aliyedhaniwa kuwa mfu kufufuka
kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali moja mjini Naivasha
umbali wa kilomita tisini kutoka mji mkuu Nairobi.
Mwanamume huyo Paul Mburu mwenye umri wa miaka 24, alipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kunywa sumu kwa lengo la kujitoa uhai,kutokana na ugomvi wa kinyumbani na babake ingawa alisemekana kufariki Jumatano usiku wakati akipokea matibabu.
Wafanyakazi wa hospitali hiyo walipigwa na butwaa na hata kutoroka walipoona mwili wa mtu aliyedhaniwa kufariki ukisonga na kuonyesha dalili za kuwa hai katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Afisaa mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo ya wilaya, Dokta Joseph Mburu, alisema kuwa dawa iliyotumiwa kumtibu Mburu hufanya moyo kupiga polepole hali ambayo huenda ilimfanya muuguzi kudhani kuwa mgonjwa alikua amefariki.
Mwanamume huyo alisikika akimtaka mmoja wa wafanyakazi katika chumba cha kuhifadhia maiti kumsaidia kwani alikuwa anahisi baridi kali na hapo ndipo mmoja wa wafanyakazi alipotimua mbio kwa hofu.
Nusura Mburu awekwe kwenye jokovu la kuhifadhia maiti.
Jamaa za mwanamume huyo akiwemo babake walikuwa wametembelea chumba cha maiti siku ya Alhamisi ili kujiandaa kwa mazishi , lakini baadaye mchana walifahamishwa kuwa Mburu alikuwa hai.
Kutoka BBC
0 maoni:
Post a Comment