Polisi wa kimataifa Interpol,
wamemuweka mwanamke aliyeshukiwa kuongoza mashabulizi ya kigaidi nchini Kenya
raia Muingereza Samantha Lewthwaite, kwenye orodha ya watu wanaosakwa sana
duniani.
Hatua hii ni kutokana na ombi la serikali ya Kenya kwa Interpol.
Bi Lewthwaite, mwenye umri wa miaka 29, ni mjane wa mlipuaji
aliyefanya shambulizi la kujitoa mhanga mjini London Uingereza mwezi Julai
mwaka 2005
Anajulikana kama "white widow", na amehusishwa na
kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini Somalia.
Polisi wa Interpol hata hivyo hawakuhusisha hatua ya kumsaka
Samantha na shambulizi la kigaidi dhidi ya jumba la maduka la Westgate mjini
Nairobi lililowaua watu 67.
Hata hivyo, hatua hii ya kumsaka Bi Lewthwaite inakuja punde
baada ya shambulizi hili la kigaidi nchini Kenya.
Al-Shabab ilikiri kufanya mashambulizi hayo yaliyotokana na
kutekwa kwa jengo la Westgate na kisha kutekwa kwa raia wa kawaida waliokuwa
ndani ya jengo hilo kwa siku nne.
Kwa mujibu wa polisi wa Interpol, mwanamke huyo anasakwa na
serikali ya Kenya kwa kumiliki mabomu na kupanga njama ya kufanya mashambulizi
kuanzia Disemba mwaka 2011.
Ikiwa mwanamke huyo atakamatwa katika nchi mwanachama wa
Interpol, atazuiliwa na kusibiri kupelekwa katika nchi anayotakikana kwa kesi
kufunguliwa dhidi yake.
Bi Lewthwaite anajulikana kwa jina bandia la, "Natalie
Webb" –na alikuwa anasakwa kwa madai ya kumiliki hati bandia ya usafiri
nchini Afrika Kusini.
Ni mjane wa Germaine Lindsay, mmoja wa washambuliaji wanne
waliohusika na shambulizi la kigaidi mjini London ambapo watu 52 waliuawa na
mamia ya wengine kujeruhiwa.
Kutoka
BBC
0 maoni:
Post a Comment