Waasi nchini ya Sudan Kusini wamesema kuwa
hawatashiriki katika awamu ya pili ya mazungumzo ya kuleta amani yaliyokuwa
yamepangiwa kuanza siku ya Jumatatu katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Waasi hao wamesema kuwa hawatarudi kwenye meza ya
mazungumzo hadi wafungwa wanne wa kisiasa waliobakia watakapoachiliwa huru.
Aidha wawakilisha wa waasi hao wanaoongozwa na
aliyekuwa makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini, Riek Machar, wamesema mbali
na wafungwa hao kuachiliwa huru, wao pia wanataka jeshi la Uganda ambalo
limekuwa likiunga mkono serikali kuondoka nchini humo, kabla ya mazungumzo hayo
kuendelea.
Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza mapigano ambayo
yamesababisha vifo vya maelfu ya watu tangu yalipoanza Desemba mwaka jana.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr amemshutumu makamu
wake wa zamani kwa kuongoza uasi ndani ya serikali na kutaka kufanya mapinduzi
ya serikali, madai ambayo yamepingwa vikali na Bwana Machar.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa mamia ya watu wameuawa
tangu mapigano hayo kuanza huku maelfu ya wengine wakilazimika kuhama makwao na
wanahitaji misaada.
Kutoka BBC
0 maoni:
Post a Comment