Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa imeipongeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kujitahidi
kutekeleza vyema majukumu yake licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo ya ufinyu wa bajeti.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu
ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Venance Mwamoto wakati akichangia
majadiliano baina ya kamati na Menejimenti ya taasisi hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa kamati yake imeweza kuona hali
halisi ya kiutendaji, hivyo atamfikishia mwenyekiti wake ili waweze kuona namna
kamati hiyo itakavyoweza kutatua changamoto hizo kwa pamoja kwa lengo la
kuiwezesha Sekretarieti ya Ajira kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wajumbe wa Sekretarieti
ya Ajira Bw. Bakari Mahiza wakati akiikaribisha kamati hiyo, mbali na kuwashukuru na kuwapongeza kwa kuchaguliwa
kusimamia sekta hii nyeti inayosimamia rasimaliwatu ambayo ni muhimu katika
taifa lolote.
''Kwa uzoefu wangu, natambua kuwa nchi nyingi
zilizoendelea ni zile zilizowekeza katika watumishi wenye sifa, ujuzi, ubunifu
na maadili mema ambao wanauwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo
za kisiasa, kijamii na kiuchumi'' Alisema Mahiza.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe.
Jason Rweikiza wakati akifungua kikao cha kamati yake na Menejimenti hiyo
amesema wameamua kutembelea Taaisis hiyo ili kujua namna inavyotekeleza
majukumu yake na kuona wanavyoweza kushirikiana kwa pamoja ili kuongeza ufanisi
wa chombo hicho.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki ameishukuru kamati hiyo
kwa kutembelea Taasisi mbalimbali zilizo chini yake na kuahidi kufanyia kazi
ushauri walioutoa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutumia fursa mbalimbali ikiwemo
makongamano ya taasisi nyingine katika kutoa elimu zaidi kwa umma, kuhakikisha
inaendelea kupunguza siku za uendeshaji wa mchakato wa ajira pamoja na kufanya
marekebisho ya Sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya kiutumishi ili kuweza
kuboresha utendaji kazi na kupunguza malalamiko yasiyo na ulazima.
Wakati huohuo, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi pamoja na kueleza jinsi Mchakato wa Ajira
unavyoendeshwa, mafanikio, changamoto na matarajio ya chombo hicho, Pia
ameahidi kamati hiyo kufanyia kazi ushauri na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa
na wajumbe wa kamati hiyo ili kuhakikisha Serikali inapata watumishi wenye
sifa, weledi kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu.
0 maoni:
Post a Comment