NYUMBA inaficha siri kubwa za wanandoa.
Ukiwaona mke na mume barabarani wakiongozana na wakati mwingine wakicheka
usifikiri wote wanaamani ndani ya mioyo yao.
Makala ya leo inatokana na simulizi niliyosimuliwa na rafiki yangu
mmoja anayeishi maeneo ya Temeke, Dar es Salaam.
Ni vizuri nikaweka hapa baadhi ya simulizi hiyo, ili nawe msomaji upate
kujua nilichosimuliwa na ikibidi utoe maoni yako.
Soma kisa
kwa ufupi:
Rafiki yangu ananisimulia jinsi wanavyoishi
maisha ya shida na mkewe kwa zaidi ya miezi miwili sasa. Shida anayosema sio
shida ya kukosa matumizi, kula wala sehemu ya kulala.
Shida anayosema ni ugomvi wake na mkewe. Ugomvi
wenyewe umesababishwa na yeye (mwanaume) kutoka nje ya ndoa, jambo ambalo mkewe
ameligundua na kuamua ‘kumsitishia huduma.’
Anasema, mkewe amegoma kumpikia, kumfulia,
kulala naye kitanda kimoja na hata kuzungumza naye. Hiyo ndiyo adhabu aliyoamua
kuitoa mwanamke kwa mumewe kwa madai kwamba, huduma hizo hata ‘kimada’ anaweza
kumpa.
Rafiki yangu anadai watazungumza na kucheka na
mkewe, labda wanapokuja wageni tu basi! Lakini wakiondoka, mkewe anarudia
kukunja ndita.
Kinachomshangaza rafiki yangu huyu ni pale
wanapofikiwa na wageni nyumbani kwao. Anasema wanapokuwa pamoja na mkewe hakuna
mgeni anayefikiri kama wana matatizo katika ndoa yao.
Anasema yeye na mkewe wanapokuwa na wageni
hukaa pamoja, huongea na kucheka utafikiri hawana tatizo. Lakini wakiingia
chumbani kwao tu mambo yanarudi kama awali.
Jamaa anashangazawa zaidi na vitendo vya mkewe anavyovionyesha wakati
anapotoka asubuhi kwenda kazini.
Anasema mkewe akimuona anatoka ndani hutangulia
kumsubiri nje na kumuaga kwa bashasha zote “kazi njema mume wangu.” Na mara
nyingi anatamka haya mbele za majerani zake.
“Unajua mshkaji wakati mwingine nikiona mke
wangu ameniaga kwa bashasha wakati usiku mzima ameninunia nahisi kama ugomvi
wetu ndio umekwisha,” anasimulia na kuongeza…
“Na hata jioni nikirudi kutoka kazini, kama
nitamkuta nje ananipokea vizuri na hasa kama kutakuwa na watu wengine, lakini
tukiingia ndani tu, mziki unakuwa uleule.”
Jamaa anasema amashaomba radhi kwa mkewe
kutokana na kosa alilolifanya lakini bado mkwewe ameendelea na msimamo wake wa
kumnyima huduma. Anasema huduma inayomuumiza zaidi kuikosa ni kuzungumza na
mkewe.
Baada ya rafiki huyu kunipa mksa wake
nikamwambia “mkeo ni miongoni mwa wanawake wachache ama waliofundwa wakafundika
au waliojifunda wenyewe.”
Akaniuliza kuninyima huduma wewe ndio unaliona
jambo zuri la kumsifia? Nikamwambia
hapana. Simsifii kwa hilo. Ninachomsifia ni tabia yake ya kutotangaza matatizo
yake na mumewe.
Hata hivyo, nikamwambia kwa kosa ulilofanya ni
lazima upewe adhabu, sasa mkeo ameamua kukupa adhabu ndogo tu ya kukunyima
huduma kimya kimya ambayo muda si mrefu ataifuta.
Nikamweleza lazima ampongeze mkewe kwa kutotoa
siri za ndoa yao. Wapo baadhi ya wanawake na wanaume wasiokuwa na siri na
hukisema kwa majerani na marafiki kila kinachofanyika chumbani.
Hekima alizonazo mwanamke huyu zinapaswa kuigwa
na wanandoa wengine wake kwa waume. Kila mtu anapaswa kujua kuwa anapotoa siri
za ndoa yake pamoja na kumdhalilisha mweziwe pia anajidhalilisha yeye mwenyewe.
Hivi ndivyo nyumba inavyoficha siri. Kama
mwanamke huyu angekuwa anapayuka ovyo kwa kumweleza kila mtu matatizo yake na
mumewe basi kila mtu mitaani angekuwa anamnyooshea kidole.
Na hata baada ya ugomvi wao kwisha, vidole
wangekuwa wananyooshewa wote wawili. Lakini kwa kuamua ‘kufa’ na siri yake
moyoni siku utakapomalizika ugomvi hakuna mtu mwingine atakayejua nje ya nyumba
yao.
Hii ndiyo siri ya nyumba ninayotaka msomaji wangu nawe uijue na
kuithamini. Ugomvi wako na mumeo au mkeo uishie ndani mwenu, hakuna sababu ya
kuwapa faida watu wengine wasio husika na ndoa yenu.
Yanini kuwapa watu faida wakati unajua kama sio kesho basi keshokutwa
hali ya amani katika ndoa yenu itarejea kama awali.




0 maoni:
Post a Comment