WILTRED RWAKATARE ATAKIWA KUJIUZULU
TAASISI ya Raia ya Haki za Kisiasa na Mwenendo wa Bunge (CPRW) imemtaka Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilfred Rwakatare, ajiuzulu wadhifa wake ili kupisha uchunguzi huru wa polisi na kutoa nafasi kwa wanachama wake kumchunguza kuhusiana na tuhuma alizokumbana nazo za kuhatarisha usalama wa nchi.
Pia kimeitaka serikali kuruhusu matumizi ya analogia kwa vyombo vya habari ili kutoa haki ya kupata habari kwa wananchi kama ilivyoanishiwa kwenye katiba ya nchi.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Marcossy Albanie, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo katika mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.
Alisema taifa limeendelea kuwa na mwenendo usioridhisha nchini juu ya shughuli za kisiasa na haki za raia katika utekeleza wa shughuli za umma na huduma za kijamii katika kujenga mustakabali wa pamoja na ustawi wa nchi katika kipindi ambacho nchi imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Viongozi wetu wanatakiwa kuwajibika kutokana na maoni ya wananchi ili kulinda heshima yao ndani ya jamii, kwa mfano suala la Rwakatare tuhuma zinazomkabili ni kinyume cha matarajio ya raia kwa nafasi aliyonayo kwenye chama kikuu cha upinzani nchini na ambacho kinaongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni.
“Kwa hiyo anatakiwa kujiuzulu nafasi yake ili kulinda heshima ya chama kama kinavyotaka viongozi wengine wawajibike pindi wanapotuhumiwa na kukosea.
“Pia kwa upande wa hili suala la uhuru wa kupata habari tunaona kuwa bado limeendelea kupigwa danadana katika kutolewa uamuzi sahihi ingawa malalamiko mengi miongoni mwa watumiaji wa runinga juu ya upatikanaji wa mawimbi ya habari kwa njia ya digitali bado haijasambaa nchini.
“Kuna taarifa kuwa kuna ving’amuzi 500,000 tu kwa mkoa wa Dar es Salaam mkoa ambao una wakazi zaidi ya milioni nne na ambapo pia kunakadiriwa kuwa na vizio vya televisheni milioni 1.5.
“Hii ni sawa na kusema katika kila watu watatu wenye vizio vya televisheni ni mtu mmoja tu ndiye mwenye kupata mawasiliano leo baada ya serikali kuzima mitambo ya analojia huku wananchi wengi wakiwa hawana uwezo wa kununu ving’amuzi,” alisema.
0 maoni:
Post a Comment