Mzozo wa kisiasa umeibuka nchini
Zimbabwe baada ya rais Robert Mugabe kutoa agizo kuwa uchaguzi mkuu nchini humo
utafanyika tarehe Thelathini na Moja Julai mwaka huu.
Waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan
Tsvangirai, ametoa taarifa muda mfupi tu baada ya agizo hilo la rais, akisema
kuwa rais Mugabe amekiuka sheria kwa kutoshirikisha bunge na ameapa kupinga
uamuzi huo.
Katika kikao na waandishi wa habari,
Tsvangirai, amemshutumu Bwana Mugabe kwa kukiuka mkataba wa ugavi wa mamlaka
uliosainiwa miaka mitano iliyopita, baada ya mzozo kuhusu matokeo ya kura
kusababisha ghasia nchini humo.
Tsvangirai ametaka uchaguzi huo
kuhairishwa hadi mageuzi ya kikatiba yafanyike ili kuhakikisha zoezi hilo la
uchaguzi linafanyika kwa njia huru na haki.
Bunge la nchi hiyo bado linajadili
mswada wa sheria ambao utaruhusu vyama vyote vya kisiasa kupewa nafasi sawa
katika shirika la habari la serikali wakati wa kampeini.
Lakini wiki mbili zilizopita
mahakama ya kikatiba nchini humo iliagiza kuwa uchaguzi huo ni sharti ufanyike
kabla ya mwisho wa Julai.
0 maoni:
Post a Comment