Nchini Tanzania, idadi
ya wakimbizi kutoka Burundi, inaendelea kuongezeka kila uchao. Umoja wa Mataifa
umesema kuwa wakimbizi mia nne kutoka Burundi huvuka mpaka na kuingia Tanzania
kila siku.
Kufikia sasa zaidi ya
wakimbizi elfu tisini wamekimbilia nchi jirani ya Tanzania tangu mzozo wa
kisiasa kuanza nchini Burundi, Aprili mwaka huu.
Idadi ya watu mashuhuri
wanaouawa nchini humo imekithiri katika siku za hivi karibu.
Akizungumza na BBC,
Mkurugenzi wa Shirika na Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini
Tanzania, Joyce Mends-Cole amesema ziko sababu kadhaa zinazowafanya wananchi
wengi wa Burundi wazidi kuikimbia nchi yao, kubwa likiwa hofu waliyo nayo juu
ya usalama wao.
Mends-Cole amesema
taarifa zinadai kuwa ingawa maeneo mengine ya Burundi yametulia bado
hakujapatikana utulivu katika mji mkuu Bujumbura, na kumekuwepo na milipuko
kadhaa ambayo inaweza kuwa chanzo cha hofu kwa wananchi wanaoikimbia nchi.
Mkurugenzi huyo wa
UNHCR amesema pia kuwa shirika hilo limekuwa na mazungumzo na wenzao walioko
Burundi kuona uwezekano wa kuwarejesha warundi nyumbani kwao lakini kwanza
wanazingatia suala la usalama wa wale wanaokimbia maeneo yasiyo na usalama.
Aidha Mends-Cole
amesema hivi sasa Kambi hiyo ya Nyarugusu inayowapokea wakimbizi hao imeelemewa
na idadi kubwa ya watu na sasa Shirika lake la UNHCR limekuwa likifanya
mazungumzo na Serikali ya Tanzania kuona kama wanaweza kuwaongezea eneo zaidi
kwa ajili ya kufungua kambi nyingine za wakimbizi.
Umoja wa Mataifa
unasema zaidi ya watu elfu tisini wameikimbia Burundi na kuingia Tanzania tangu
kuanza kwa vurugu mwezi wan ne mwaka huu.
Mwezi uliopita
aliyekuwa afisa mkuu wa idara ya upeleleza Adolphe Nshimirimana aliuawa, baada
ya gari lake kushambuliwa kwa grunedi na watu wasiojulikana.
Chanzo BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment