MWERA AMAZING BLOG

MWERA AMAZING BLOG
SERIKALI imetakiwa kutoa kipaumbele katika kuboresha elimu ya awali kwa kutenga bajeti ili kuinua kiwango cha elimu nchini.
Pia imetakiwa kutekeleza ahadi ya kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa elimu ya awali ili wasiingiliane na wale wa shule za msingi.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya elimu nchini (HakiElimu), Elizabeth Missokia, wakati akizindua kampeni ya kuboresha elimu ya awali nchini.
Alisema serikali imekuwa ikionesha umuhimu wa elimu ya awali pindi inapotamka pekee kwa sababu ahadi nyingi hazitekelezwi kama inavyotakiwa.
“Kwa mfano serikali imeahidi kuwa kila shule ya msingi iwe darasa la elimu ya awali lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo, pia iliahidi kuandaa walimu wengi wa elimu ya awali na kuwapanga katika shule zinazohusika.
“Lakini cha ajabu hadi sasa hakuna uwiano wa walimu na wanafunzi kwa sababu tafiti zinaonesha kuwa mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 111 badala ya 25, wakati huo huo kiwango cha watoto wanaojiunga na elimu ya awali ni kidogo sana kwa sababu asilimia 42 peke ndio wanaojiunga na elimu ya awali kabla ya kuendelea na ya msingi.
“Licha ya ahadi nyingi za serikali kwa mfano katika kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu ya awali pamoja na makubaliano tuliyojiwekea kati ya wadau na serikali, tumeona kuwa haijatenga kabisa bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu hiyo.
“Hili linatupa wasiwasi wadau wa elimu kama kweli serikali ina nia ya dhati kuboresha elimu ya awali nchini au bado inaendelea kuja na mikakati ambayo haina utekelezaji,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi na Makuzi kwa Watoto Tanzania (TECDEN), Arcard Rutajwaha, alisema wazazi nao wanatakiwa kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya watoto wa elimu ya awali nchini.
“Kwa sababu baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaachia walimu jukumu la kulea watoto, wakati wanajua jukumu kubwa la mwalimu ni kumkuza mtoto kiakili pekee.
“Kwa mfano kuwaandalia stadi za kazi kwa ajili ya kujifunza kwa kuimba, kusoma na kuandika, muda wa umri wa mtoto kuanzia mwaka 0 hadi 8, ni umri ambao kila mmoja anatakiwa kuwajibika ili kukuza upeo wa watoto.
“Watoto wanatakiwa kukua huku wakijifunza mila, utamaduni na tabia za wazazi wake,” alisema.
Alisema kampeni hiyo ilipewa jina la ‘boresha elimu ya chekechea’ inalenga kuitaka serikali itimize ahadi na wajibu wake wa kutoa elimu bora kwa wananfunzi wote wa elimu ya awali ambayo ni muhimu sana katika kujenga msingi imara kielimu.
Share on Google Plus

About MWERA AMAZING

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 maoni:

Post a Comment