KATIKA kuadhimisha sikukuu ya wapendano (Valetine)
Wanachama wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Dar es Salaam
wametoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni mbili kwa
wagonjwa wa hospitali ya Mwananyamala.
Wakikabidhi msaada huo jana wanachama hao waliokuwa
wameambatana na viongozi mbalimbali wa chama hicho, pia walifanya usafi katika
hospitali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Diwani wa Kata ya Ubungo
Boniface Jacob, alisema wametumia maadhimisho hayo katika kuwafariji wagonjwa
wa hospitali hiyo.
“Moja ya sera ya Chadema ni upendo kwa umma na uzalendo kwa
Taifa na ndio tafsiri ya rangi nyekundu iliyopo kwenye bendera yetu. Tumechagua
siku ya wapendanao kuonesha kwa vitendo namna tunavyoupenda umma wa Watanzania
na tunawafariji wagonjwa kwa kuwa kila mwananchi anayothamani bila kujali hali
yake kiafya.
“Tunafanya hivi huku tukifahamu kwamba CCM kimetelekeza
uduma za afya imewatupa watumishi katika sekta hii nyeti kwa kutowalipa maslahi
yao stahiki, kukiwa na uhaba wa madakatari na wauguzi.
“Tunafanya hivi ili pia kuunga mkono jitihada za Wabunge na
Madiwani wa Chadema ndani ya manispaa ya
Kinondoni za kuboresha huduma za afya za wananchi wa ngazi zote.
“Wabunge na madiwani wetu wamekuwa wakipigia kelele ukosefu wa vitanda, upungufu watumishi na
ubora wa huduma katika hospitali na zahanati zilizopo ndani ya Manispaa ya
Kinondoni na hususani Hospitali ya Mwananyamala,” alisema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Ngonyani Sophinias, alishukuru wanachama hao kwa msaada huo na kutoa wito kwa watu wengine
kuisaidia sekta ya afya nchini.
“Kuna changamoto nyingi sana katika sekta ya afya nchini,
hivyo ni vyema kwa Watanzania pamoja na watu wengine kujitoa kuisaidia sekta
hii,” alisema.
0 maoni:
Post a Comment