Polisi nchini Norway wanamchunguza
Hassan Abdi Dhuhulow, kuhusu shambulio la kigaidi katika kituo cha biashara cha
Westgate nchini Kenya karibu mwezi mmoja uliopita.
Mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 23, raia wa Norway mwenye
asili ya Somalia, anashukiwa kusaidia mpango wa kufanyika kwa shambulio hilo.
BBC imezungumza na mmoja wa ndugu wa mtuhumiwa aliyeko nchini
Norway, ambaye amesema, Hassan Abdi Dhuhulow aliondoka kutoka mji wa Larvik
kwenda Somalia mwaka 2009.
Watu wapatao 67 waliuawa katika shambulio hilo mjini Nairobi,
ambapo kundi la al-Shabaab lenye uhusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda
lilikiri kuhusika na shambulio hilo.
Wiki iliyopita shirika la ujasusi la Norway, PST, lilisema kuwa
limewatuma maafisa wake nchini Kenya kuthibitisha taarifa hizo kwamba raia wa
Norway alihusika katika shambulio la Westgate, lililoanza tarehe 21 Septemba na
kudumu kwa siku nne.
Bado haijafahamika ni wapiganaji wangapi walihusika. Awali
polisi wa Kenya walikadiria kuwepo kwa washambuliaji kati ya 10-15 katika kituo
cha kibiashara cha Westgate, lakini picha za CCTV ambazo zimekwishatolewa na
serikali ya Kenya, imewaonyesha washambuliaji wanne.
Hassan Abdi Dhuhulow anaaminika kuwa mmoja kati ya watu wanne
walionekana katika picha za CCTV.
Wachunguzi wa vinasaba bado wanaendelea na kazi ya uchambuzi wa
mabaki na vifusi katika eneo la Westgate na hakuna miili zaidi iliyogundulika
na haifahamiki kama washambuliaji hao waliuawa au bado ni hai.
Kutoka BBC
0 maoni:
Post a Comment