Soma hii Taarifa kutoka Mbeya City FC, juu ya tuhuma
za kupokea mkwanja kutoka kwa timu ya Azam FC………
Kwanza nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati
wapenzi wote wa mchezo wa mpira wa miguu na wapenzi wa Mbeya City Fc popote
pale walipo kwa kuiunga mkono timu yao muda wote wa michezo ya ligi kuu
inayoelekea ukingoni hivi sasa.Klabu inathamini nafasi ya wapenzi na washabiki
katika kujenga timu imara na yenye ushindani kama walivyofanya kwa timu yetu.
Timu yetu ilianza ligi msimu huu 2013/2014 ikiwa na
malengo ya kuchukua ubingwa au kuwa katika nafasi za juu za ligi yetu.Hiyo
ndiyo dhamila iliyokuwepo kwa viongozi,wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Michezo miwili imesalia kwa timu yetu kabla ligi kuu
ya Vodacom kumalizika katika msimu huu 2013/2014.katika safari yetu ya ligi kuu
kwa mara ya kwanza msimu huu, changamoto nyingi za kiutawala na za kimtazamo
kutoka kwa wadau wote wanaohusika na mchezo wa mpira wa miguu nchini
tumezishuhudiaChangamoto hizo ikiwemo upangaji wa ratiba usiokuwa na uwiano
mzuri.
Baadhi ya mechi kuamuliwa vibaya na waamuzi wa mchezo,
wizi wa mapato ya milangoni unaotokana na mfumo mbaya wa uuzaji wa tiketi,
uadilifu mdogo kwa baadhi ya viongozi wenye dhamana ya kusimamia mpira katika
ngazi zote n,k.
Kuelekea mchezo wetu wa tarehe 13/04/2014 dhidi ya
AZAM FC kumezuka propaganda chafu na ambazo si sahihi katika ukuzaji wa mpira
hasa wa ligi ndogo kama ya Tanzania.
Nachukua nafasi hii kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo
ambayo yamekuwa sehemu ya propaganda hizo:
1. Klabu imehaidiwa kununuliwa na inajiandaa
kutoa ushindi kwa kwa timu ya AZAM Fc na kuwarahisishia mazingira ya Ubingwa.
Halmashauri ya jiji la Mbeya limekuwa katika mchakato
wa kutafuta na kununua basi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya
Halmashauri ikiwemo kutumiwa na timu zake ( Netiboli na Mpira wa miguu)ambazo
zote zipo ligi kuu ya michezo husika kwa kufuata sheria ya manunuzi ya Umma.
Mchakato huo ulianza tarehe 8/8/2013 halmashauri
ilipotangaza nia hiyo katika gazeti la “the guardian” la tarehe hiyo kwa tender no.LGA/069/2013-2014/MCC/G/01 hii
ni baada ya Halmashauri kutenga bajeti ya fedha za makusanyo yake ya
ndani kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na 2013/2014 ili kukidhi haja hiyo.
Tangazo hilo halikupata mzabuni mwenye sifa za kufanya
usambazaji wa basi hilo hivyo tangazo hilo lilirudiwa tena tarehe 12/2/2014
katika gazeti la majira kwa Tender No.LGA/069/2013-2014/MCC/G/01
(Re-advitised), Mchakato na maandalizi ya ufunguaji wa ufanyaji
wa tathmini wa zabuni hiyo unaendelea kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya Umma.
Pamoja na mchakato huo hapo juu,pia klabu inaendelea
na mazungumzo na wadau mbalimbali wenye nia ya kuwekeza kwa udhamini wa bidhaa
zao,moja ya maeneo ya udhamini ni pamoja na ununuzi wa basi la wachezaji
taratibu na makubaliano haya yatakapo kamili umma wa wapenda mchezo wa mpira wa
mguu utajulishwa.
Hivyo propaganda hiyo kuwa klabu imehongwa basi si za
kweli na si sahii ila zina nia ya kuidhalilisha timu yetu.
2. Propaganda kuwa Mwalimu Juma Mwambusi
kanunuliwa nyumba Maeneo ya chamazi ili apange kikosi dhaifu siku ya mchezo
tarehe 13/4/2014.
Mwalimu(Kocha) Juma Mwambusi ni muajiliwa wa
Halmashauri ya jiji la Mbeya,kwa maana hiyo ni mtumishi wa Umma. Mwalimu
Mwambusi amekuwa na timu yetu kwa muda mrefu sasa na ataendelea kuwepo.Kumekuwepo
na maneno yasiyofaa dhidi ya mwalimu wetu toka mzunguko wa pili wa ligi kuanza.
Maneno haya yamekuwa na nia ya kuaribu muenendo wa
timu ili ianze kufanya vibaya lakini zaidi ya hapa yana nia ya kumdhalilisha
mwalimu wetu na taaluma ya ukocha nchini.
Mwalimu amefedheheshwa sana na taarifa hizo.
3. Propaganda kuwa wachezaji wote wa kikosi cha
kwanza wamepewa hongo wacheze chini ya kiwango 13/4/2014.
Wachezaji ndiyo wachezaji wenye nidhamu kubwa katika
ligi ya mwaka huu ndani na nje ya uwanja muda wote,ni waadirifu na wanajua
wanataka nini.Mpira ndiyo ajira yao kama watumishi wa umma ndani ya Halmashauri
ya jiji la Mbeya.Hawajawahi na wala hawatawahi kuchukua rushwa kwa lengo la
kupanga matokeo.
Klabu yetu haisadiki katika upangaji wa matokeo ya
mchezo wa mpira wa miguu kwani tunajua fika kuwa hakutaisadia kama klabu lakini
pia kama taifa katika kuendeleza mpira wa
miguu nchini.
Hitimisho,
Mchezo wa mpira wa miguu una matokeo matatu
kushinda,kushindwa na kutoka sare. Klabu inaamini kuwa timu iliyojiandaa vizuri
kama yetu inastahili kupata matokeo mazuri
uwanjani.Falsafa mojawapo ya timu yetu ni kushinda mechi kwa kucheza mpira
unaovutia na kuwaburudisha watazamaji.
Tuhuma mbalimbali za upangaji matokeo katika ligi yetu
zimeanza kuota mizizi hasa ligi inapoingia mzunguko wa pili ,katika suala hili
kama ambavyo linataka kuhusishwa nasi yawezekana propaganda hizi kwa upande wa
timu inayotuhumiwa kuandaa michakato hiyo wana uzoefu nalo na yumkini ndiyo
chachu ya mafanikio yao
mpaka kufikia hatua hiyo waliofikia sasa.
Kama timu hiyo inauwezo wa kirasilimali wa kufanya uovu
huo wote iweje ishindwe kuwa na timu imara na ya ushindaji mpaka itegemee
kutafuta wachezaji wa timu pinzani kupata matokeo mazuri?
Timu yetu ndiyo timu pekee changa miongoni mwa timu
tano zinazoongoza msimamo wa ligi yetu kwa sasa,si hivyo tu bali ndiyo timu
pekee inayoundwa na wachezaji wengi wapya katika ulimwegu wa soka na inayoundwa
na Watanzania watupu kuanzia wachezaji,benchi la ufundi pamoja na viongozi.Hii
inathibisha kuwa kama taifa tunaweza kufanya kazi nzuri bila kutegemea
wachezaji toka nje baadhi yao wasiokuwa na tija.
Mpira ni ajira hatuna budi kuuratibu vema ili kutoa
nafasi inayostahili kwa vijana wetu ili kupunguza tatizola ajira nchini lakini
pia kutumia vipaji vyao kulipa taifa muonekano stahili.
Mamlaka zinazohusika hazina budi kuanza kufuatilia na
kuchukua hatua kali kwa baadhi ya timu zinzohusishwa na upangaji wa matokeo ili
kulinda heshima ya mchezo huo bila kuogopa uwezo wa rasilimali wa timu hizo.
E.E.Kimbe
KATIBU MKUU
MCC FC
9.04.2014
0 maoni:
Post a Comment