MWERA AMAZING BLOG

MWERA AMAZING BLOG
MTANDAO wa Asasi za Kutetea Haki za Binadamu unatarajia kuitisha maandamano nchi nzima kupinga ukatili aliofanyiwa Dk. Stephen Ulimboka, wanaharakati wengine na kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi.
Pia umevitaka vyombo vya habari kuacha kuandika habari zinazowahusu viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, na hata ikiwezekana pia na Serikali kwa ujumla iwapo itaendelea kupuuza kulifungulia gazeti hilo.
Tamko hilo limetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya kushughulikia sakata la Dk. Ulimboka na gazeti la Mwanahalisi, Marcossy Albanie, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio hayo.
Alisema mtandao huo umetoa siku saba kwa serikali kulifungulia gazeti la hilo na kufanyia kazi yale yalibainishwa na gazeti hilo kabla haujachukua hatua zaidi.
“Tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali kulifungulia mara moja na bila masharti gazeti hili ambalo limekuwa kipenzi cha wananchi. Tunaitaka serikali ndani ya siku saba kutekeleza hili kwa kuangalia maslahi mapana ya jamii badala ya kuangalia maslahi ya baadhi ya viongozi wenye maisha fulani katika kutimiza malengo yao binafsi.
“Serikali itekeleze takwa hili haraka iwezekanavyo na kwamba asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu ya wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu tatu.
“Kwanza sheria ya magazeti hairuhusu ukataji wa rufaa kwa waziri wa habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kuhukumu gazeti bila kutoa nafasi kwa wahusika kusikilizwa, pili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na sheria hiyo kutomtaja, hakueleza kuwa yuko tayari kupokea malalamiko ya Mwanahalisi, hivyo kutoeleza kwake tunachukulia kama njia ya kukwepa wajibu wake.
“Tatu hatukubaliani na kauli ya waziri mkuu na wengine wanaotaka Mwanahalisi waende mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa serikali haukutumia njia ya mahakama kulifunguia gazeti hilo, ndio maana tunaona serikali inataka kuitumia mahakama ili kuchelewesha gazeti hilo kupata haki yake,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania, (MISA Tan), Mohamed Tabanyendera, aliitaka serikali, badala ya kushughulika na watetezi wa haki na wanahabari wanaofichua uovu, ishughulike na wahalifu waliomteka, kumtesa na hatimaye kumtelekeza Dk. Ulimboka.
“Ushahidi uliobainishwa na gazeti hili haukuacha shaka yeyote juu ya waliohusika na sakata hili, na kama serikali au watendaji wake waliotajwa wana mashaka wangetumia ushahidi wa taarifa zile kutafuta haki zao, kwa nini wasiende mahakamani au wajitokeze na ushahidi wa kukanusha yaliyobainishwa?
“Serikali iachane kabisa na ukandamizaji huu wa haki na uhuru wa habari, matendo aliyofanyiwa Dk. Ulimboka, habari zilizobainishwa na Mwanahalisi juu ya sakata hili na kufungiwa kwa gazeti hili kunaonesha mtiririko wa matukio ya serikali kuminya uhuru wa haki,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa MISA Tan, Tumaini Mwailenge, aliwataka wanaharakati  wote wasichoke wala kurudi nyuma katika azma ya kutete haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.
“Fedha zipo kwa ajili ya kuwaficha watetezi au waandishi wote watakaotishiwa maisha yao kutokana na harakati hizi, hivyo tunao uwezo wa kufanya lolote tunawaomba waandishi wa habari mtusaidia katika hili,” alisema..
Julai 30 mwaka huu, serikali kwa kupitia wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo ilitangaza kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la Mwanahalisi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi zinazohatarisha amani na utulivu nchini
Share on Google Plus

About MWERA AMAZING

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 maoni:

Post a Comment