Malema azuiwa kuhutubia wachimba migodi
Mwanasiasa
tatanishi nchini Afrika Kusini Julius Malema amezuiwa kuwahutubia wafanyakazi
wa migodini wanaogoma katika mgodi wa Marikana.
Takriban wachimba
migodi 2,000, walikusanyika katika uwanja mmoja ulioko karibu na mgodi huo
Kaskazini Magharibi mwa Johannesburg
kumsikiliza Malema.
Migomo ya wachimba
migodi ambayo inakumba nchi hiyo tayari imeathiri uzalishaji wa madini ya
dhahabu na Platinum katika nchi hiyo ambayo ina utajiri mkubwa wa maliasili.
Rais Jacob Zuma
amesema kuwa hatua ya wachimba migodi imesababisha hasara ya karibu dola
milioni 548 kwa sekta ya madini.
Akiongea kabla ya
kongamano la vyama vya wafanyakazi nchini humo, (Cosatu) Zuma alisema kuwa
migomo ya mwaka huu imekosesha hazina ya fedha dola milioni 388.
Wiki jana serikali
ilisema kuwa itachukua hatua za dharura dhidi ya wale wanaochochea fujo na
hivyo kuisababishia sekta ya madini mamilioni ya hasara.
Baada ya
kutofautiana na polisi waliokuwa wanalinda uwanja huo, Malema alisindikizwa na
kikosi maalum cha polisi hadi mbali sana
na uwanja huo. Magari mawili ya polisi yenye silaha yalifuata gari la Malema na
juu angani kukawa na helikopta iliyokuwa inamfuata pia.
Ametoa wito wa
maandamano ya kitaifa baada ya hapo awali, kusema kuwa shughuli za migodi
lazima zitatizwe.
Malema amekosolewa
na wengi ambao wanamuona kama mwenye njama ya
kutumia masaibu ya wafanyakazi wa migodini kujinufaisha kisiasa hasa baada ya
wachimba migodi 34 kuuawa na polisi wakati wa mgomo wao katika mgodi wa
Marikana mwei jana.

0 maoni:
Post a Comment